Na Julius Konala,
Songea.
WANANCHI wanaoishi katika kata ya Mpitimbi wilaya ya Songea
mkoani Ruvuma, watanufaika na mradi wa visima vya maji ambavyo ujenzi wake
unaendelea kufanyika katika kata hiyo na kwamba mpaka kukamilika kwake, vitaweza
kuwafanya waweze kuondokana na adha ya upatikanaji wa maji ambayo imekuwa
ikiwatesa kwa muda mrefu sasa.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Diwani wa kata hiyo, Dionis
Mang’omes wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa ambapo
alisema ni visima 24 vya maji ya kupampu, ambavyo vinajengwa katika kata hiyo.
Mang’omes alisema kuwa mradi huo ambao unafadhiliwa na
shirika la Times Life kupitia shirika la Watawa wa Benedictine wa Hanga,
utawanufaisha wananchi wa vijiji vya Mpitimbi A na Mpitimbi B vilivyopo katani
humo.
“Awali mpango ulikuwa ni wa kuchimba visima saba, lakini
kutokana na ushawishi wangu kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Peramiho
ambaye pia ni Waziri wa kazi, sera, ajira, walemavu na vijana Jenista Mhagama,
shirika hilo limeweza kuongeza idadi ya visima mpaka kufikia ishirini nne”, alisema
Mang’omes.
Alieleza kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017 wanatarajia
kuanza ujenzi wa mradi wa maji ya mtiririko katika vijiji viwili vya Mpitimbi A
na Lipaya, jambo ambalo hadi kukamilika kwake litakuwa pia limepunguza usumbufu
wa wananchi hao, kutembea umbali mrefu kufuata maji hususani kwa akina mama na
wanafuzi waliopo katika vijiji hivyo.
Pamoja na mambo mengine, amewaomba wananchi wa kata ya
Mpitimbi kujenga utamaduni wa kutunza miundombinu ya maji ambayo imejengwa kwa
gharama kubwa, badala yake watoe ushirikiano kwa serikali na viongozi
mbalimbali wa kata hiyo katika kuwafichua wale wote watakaoendesha vitendo
hivyo vya uharibifu.
No comments:
Post a Comment