Na Julius Konala,
Songea.
MBUNGE wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas Gama ametoa
msaada wa magari mawili ikiwemo la kubebea wagonjwa kwa ajili ya kusaidia
wananchi wa jimbo hilo kwenda hospitali, pale wanapougua au kuzidiwa na
magonjwa mbalimbali.
Msaada huo ulitolewa na Mbunge huyo kwenye hafla fupi
iliyofanyika uwanja wa michezo wa Majimaji uliopo mjini hapa, ikishuhudiwa na
wananchi ambao walihudhuria hafla hiyo.
Gama alisema kuwa ameamua kununua magari hayo, kupitia mkopo
ambao atakuwa anakatwa kwenye mshahara wake kutokana na kuguswa na changamoto
zinazowakabili baadhi ya wananchi wake, ikiwemo baadhi yao kutokuwa na uwezo wa
kukodi magari ya kuwapeleka hospitali kupata matibabu pale wanapougua ghafla.
"Ndugu zangu nimeamua kununua magari haya ili yaweze
kuwasaidia hata kubebea miili ya marehemu waliofariki dunia, hasa pale mnapokumbwa
na matatizo ya ukosefu wa usafiri", alisema Gama.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, alisema kuwa
katika kipindi cha miaka mitano cha uwakilishi wake atahakikisha anajitahidi pia
kupunguza kero na changamoto mbalimbali, ambazo zinawakabili wananchi wake
ndani ya jimbo la Songea mjini.
Mbunge huyo amewaomba wananchi wa jimbo hilo, kumpa
ushirikiano katika utendaji wake wa kazi kwa lengo la kusukuma gurudumu la
maendeleo ya jimbo hilo kwa uharaka zaidi.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Songea, kwa
nyakati tofauti walimshukuru na kumpongeza Mbunge wao wakieleza kwamba msaada
huo utakuwa mkombozi mkubwa kwao hasa akina mama wajawazito, watoto, wazee na
vijana.
No comments:
Post a Comment