Na Steven Augustino,
Tunduru.
MAHAKAMA ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imemwachilia
huru Mmanga Abdalah Hamdani (47) ambaye ni mtuhumiwa wa kosa la ubakaji, mtoto
wa miaka 13 wa darasa la sita shule ya msingi Nanjoka wilayani humo.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu mkazi mfawidhi Mahakama hiyo, Gladys
Barthy alisema kuwa mahakama hiyo imechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha na
ushahidi uliotolewa na wataalamu wa utabibu, mganga wa hospitali ya serikali ya
wilaya ya Tunduru Dkt. Gaofrid Mvile kuwa mtoto huyo hakubakwa.
Akifafanua hukumu hiyo, Hakimu huyo alisema kuwa kufuatia
hali hiyo mahakama imeamua kutenda haki kwa kutoa uamuzi huo wa kumwachilia
huru kwa madai kwamba, huenda binti huyo alimsingizia mbakaji huyo ambaye ni
mjomba wake kwa lengo la kutaka kumkomoa.
Akinukuu taarifa ya ushahidi uliotolewa na Dkt. Mvile, Hakimu
huyo alisema kuwa taarifa zinaeleza kuwa hadi siku wanamfanyia vipimo vya
ukaguzi wa kuthibitisha tukio hilo la ubakaji, malalamikaji hakuonesha kuwa na
dalili za kuingiliwa na badala yake alionekana kuwa na bikra yake na kwamba
kilichobainika katika uchunguzi huo ni uwepo wa mrundikano wa damu, ambazo
zilitolewa kwa kumfanyia upasuaji wa tumbo lake.
Kwa mujibu wa taarifa za awali za tukio hilo, zinaeleza kuwa
mtuhumiwa huyo alikuwa na tabia ya kumuingilia kimapenzi mtoto huyo ikiwemo pia
kinyume cha maumbile, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Awali akimsomea shitaka hilo lenye jalada namba 23/2016,
mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, mwendesha mashtaka wa Polisi Inspekta
Songelaeli Jwagu alisema kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo, February 21
mwaka huu majira ya saa 4.40 usiku baada ya kumvamia na kumziba
mdomo mtoto huyo na kufanikisha adhma hiyo.
Alisema kwa kufanya hivyo, alifanya kosa kinyume cha sheria
namba 130 (1) na (2c) ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa
mabadiliko mwaka 2002.
Katika utetezi wake mtuhumiwa huyo katika kuthibitisha kuwa
hakufanya kosa hilo, alipeleka mahakamani hapo mashahidi watatu huku Daktari
huyo ambaye alipelekwa na upande wa Jamuhuri kati ya mashahidi wake
watano ili kuweza kuthibitisha hilo.
Wakizungumzia adhabu hiyo nje ya mahakama, mama mazazi wa mtoto
huyo Fatuma khalifa Msaka na bibi wa mtoto huyo Zaituni Rashid
walidai kuwa hukumu hiyo haijawatendea haki, hivyo kutokana na wao ni familia
maskini wanamwachia Mungu.
Walisema uwepo wa matumizi mabaya ya fedha (Rushwa) ulianza
kujionesha tangu mwanzoni mwa kesi hiyo baada ya Polisi katika kituo cha wilaya
hiyo, kumwachilia huru mtuhumiwa jambo ambalo liliwafanya kulalamika kwa Kamanda
wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji ambaye aliingilia kati suala hilo
na kutoa msukumo wa kumkamata tena mtuhumiwa huyo na kesi yao kwenda
mahakamani.
Walisema shauri hilo lilifunguliwa February 21 mwaka huu na
kupewa namba TUR/IR/202/2016 lakini kilichowashangaza mtuhumiwa huyo
aliachiliwa kwa dhamana, wakati mgonjwa akiwa bado amelazwa hospitali na hali yake
ikiwa mbaya.
Katika maelezo ya nyongeza, bibi Rashid alisema kuwa kutokana
na mjukuu wake kufanyiwa tukio hilo na kuharibiwa vibaya katika maumbile yake
ya uzazi, hivi sasa amekuwa akitokwa na kinyesi na haja ndogo bila kujizuia.
Wanafamilia hao wameiomba serikali, taasisi na mashirika
ya kusimamia haki za wanawake na watoto kuwasaidia kwa kuwapatia usimamizi wa
karibu ili kesi hiyo iliyovurugwa kwa nguvu ya fedha, ifufuliwe upya ili mtoto
huyo aweze kupata haki zake za msingi.
Kwa mujibu wa taarifa za wanafamilia hao zinaeleza kuwa,
mtuhumiwa Hamdani alianza kuishi na mtoto huyo mwaka 2013 baada ya shangazi wa
mtoto huyo ambaye ni mke wa mtuhumiwa huyo, aliyetajwa kwa jina la Khadija Pemba
kwenda kumchukua katika kijiji cha Namasakata wilayani Tunduru kwa lengo la
kuishi naye.
No comments:
Post a Comment