Na Mwandishi wetu,
Namtumbo.
WAKULIMA wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, wametakiwa
kutokatishwa tamaa kutokana na changamoto mbalimbali zinazolikabili zao hilo,
badala yake waongeze juhudi katika uzalishaji wake hatua ambayo itawawezesha kuinua hali
zao za maisha.
Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri
ya wilaya hiyo, Alli Mpenye alipokuwa akifafanua juu ya mikakati mbalimbali ya
kufufua zao hilo kwa waandishi wa habari, ofisini kwake.
Aidha Mpenye alibainisha kuwa, tatizo la kushuka kwa
uzalishaji wa zao la tumbaku wilayani humo katika miaka ya hivi
karibuni kumechangiwa na wakulima kukatishwa tamaa na viongozi wa vyama vya
ushirika wilayani humo, ambao walishirikiana na makampuni
yanayonunua tumbaku kuwaibia wakulima na hata wakati mwingine kuwabambikia
madeni makubwa ya pembejeo.
Kadhalika ameishukuru serikali kuanza kuwachukulia hatua za
kisheria viongozi wote waliohusika kutafuna fedha za wakulima hao, na wale
walioua vyama vya ushirika ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo walishiriki kwa namna
moja au nyingine kuua zao la tumbaku kwa kufanya vitendo visivyofaa dhidi ya
wakulima.
Alisema kuwa, vitendo hivyo vimechangia kuwakatisha tamaa
wakulima ambao wengi wao walishakataa kurudi tena kulima zao hilo,
lakini kutokana na hatua nzuri ya serikali kuanza kuwachukulia hatua
wezi hao hivi sasa baadhi ya wakulima wamekubali kuanza tena uzalishaji wa zao
hilo, ambalo miaka ya nyuma lilikuwa mkombozi mkubwa kiuchumi kwa wananchi wa
Namtumbo.
Katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo alieleza kuwa halmashauri
imeanza mkakati wake wa kulima zao la kahawa na kwamba zaidi ya miche 16,000
imenunuliwa kutoka kituo cha utafiti wa kahawa cha Ugano, kilichopo wilayani
Mbinga mkoani humo na kusambaza kwa wakulima katika kata ya Namabengo na
Msindo.
Alifafanua kuwa lengo la Halmashauri hiyo, ni
kwamba kuwa na mazao matano ya biashara ambayo yatasaidia wananchi kuondokana
na umaskini kwa sababu watakuwa na mazao mengi ya biashara, badala ya kutegemea
zao la tumbaku na ufuta.
Mpenye aliyataja mazao hayo ni ufuta, mbaazi, korosho, kahawa
na mhogo ambapo kwa mwaka ujao wanatarajia kuongeza mazao mengine mawili ambayo
ni ya choroko na viazi vitamu hivyo tayari Halmashauri, imetenga zaidi ya
shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo wilayani humo.
Pamoja na mambo mengine, wakulima wa wilaya ya Namtumbo
wamehimizwa pia kulima zao la ufuta mweupe ambalo litawaingizia
kiasi kikubwa cha fedha kutokana na zao hilo, kuwa na soko kubwa ndani na
nje ya nchi.
Halmshauri hiyo imekwisha toa mbegu 560 bure za
ufuta na kuzigawa kwa wananchi, ili waweze kufanya uzalishaji wa zao hilo la
ufuta.
Alizitaja kata zilizopata mgao huo kuwa ni Mchomoro, Namtumbo,
Mgombasi, Luchiri, Mkongo, Limamu, Likuyu seka, Rwinga, Litola, Ligera na
Namabengo ambapo hivi sasa mashamba yanaendelea vizuri na
kinachosubiriwa ni kazi ya ukataji na ukaushaji kabla ya kufungua
rasmi soko la zao hilo katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Namtumbo.
No comments:
Post a Comment