Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, limesema miili ya watu 11
ambao wahofiwa kufa maji katika ziwa Nyasa wilayani Nyasa mkoani humo, kufuatia
boti walilokuwa wakisafiria kupoteza muelekeo bado haijapatikana hivyo serikali
imeongeza maboti matatu, ambayo yatafanya kazi ya kuendelea kutafuta miili hiyo
katika ziwa hilo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji. |
Akizungumza na mwandishi wetu Kamanda wa Polisi wa mkoa huo,
Zubery Mwombeji alisema kuwa ni siku ya nne sasa imepita tokea tukio hilo
lilipotokea Mei 20 mwaka huu majira ya jioni, wakati watu hao wakitokea mji wa
Mbamba bay kwenda nchi jirani ya Malawi wakiwa kwenye boti ndogo la mizigo.
Mwombeji alifafanua kwamba wameweza kuyapata majina ya watu
hao wanaohofiwa kupoteza maisha katika ziwa hilo baada ya ndugu zao kujitokeza
na kuweza kuyataja kuwa ni, Benjamin Seme (41) na Florian Mwamlenga (31) wote
wakazi wa wilaya ya Kyela mkoani Mbeya.
Aliwataja wengine kuwa ni Ashura Shaban (33) mkazi wa Mbinga
mjini, Glory Kaunda (36) mkazi wa kijiji cha Liuli, Ramadhan Mfaume (44),
Jordan Komba (41), Seleman Mussa (41), Mkwanya Vicheko (41), Haji Jailosi (36),
Geofrey Butaya (31) na Lucas Seleman (26) wote wakazi wa Mbamba bay wilayani
Nyasa.
“Bado tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wa Malawi ili tuweze
kujua hatma ya jambo hili kufuatia mpaka sasa licha ya kufanya jitihada ya
kutafuta miili ya watu hawa, lakini bado haijapatikana hivyo tutakapokamilisha
kazi ya kuitafuta totatoa taarifa kama wamepatikana au la”, alisema Mwombeji.
Awali Kamanda huyo wa Polisi alisema kuwa kuzama kwa boti
hilo kulitokana na kuzidiwa na upepo mkali na hali ya ziwa hilo kuchafuka,
kulikosababishwa na dhoruba kali na kwamba hata boti hilo lililozama nalo bado
halijapatikana.
No comments:
Post a Comment