Mkurugenzi mtendaji Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Venance Mwamengo upande wa kushoto, akizungumza
na wakulima wa zao la Mhogo kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera
wilaya humo ambapo aliahidi kuwasaidia fedha, kwa ajili ya kununulia mashine ya kisasa
kusindika zao hilo na mazao mengine.
Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
MKURUGENZI Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma Venance Mwamengo, amewataka viongozi waliopo katika vikundi
vya wakulima wilayani humo kuwa waaminifu na waadilifu ili kuvifanya vikundi
hivyo viweze kufikia malengo yake yaliyokusudiwa na kuweza kupunguza kero na
matatizo mbalimbali, yanayowakabili wakulima waweze kuondokana na umaskini au
ukosefu wa ajira.
Mwamengo alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki, alipokuwa
akizungumza na wakulima wa kikundi cha Jitegemee ambacho hujishughulisha na
kilimo cha mbaazi, mhogo, mahindi na alizeti katika kijiji cha Kigonsera
wilayani humo huku akisisitiza kwamba uaminifu wa viongozi hao utasaidia
kwa kiasi kikubwa vikundi hivyo kuwa endelevu.
Alisema serikali imekuwa ikivisaidia fedha na hata
ushauri kwa kuwapeleka huko watalaamu wake, lakini tatizo kubwa
lililopo viongozi wasiotambua wajibu wao katika vikundi wamekuwa kikwazo
kikubwa kutokana na kutaka kujinufaisha kupitia mgongo wa wenzao kwa manufaa
yao binafsi, jambo ambalo huchangia kwa kiasi kikubwa visiweze kusonga
mbele.
Kadhalika amewataka wakulima kutokatishwa tamaa kutokana na
changamoto wanazokutana nazo katika sekta ya kilimo, bali waendelee kuongeza
juhudi na uzalishaji wa mazao shambani ili waweze kupiga hatua mbele kiuchumi.
Aidha Mwamengo, amesikitishwa na tabia ya baadhi ya watu
kutumia muda wao mwingi kukaa vijiweni kucheza bao au kunywa pombe saa za
kazi badala ya kujikita zaidi katika shuguli za maendeleo, ambapo
alisema serikali itahakikisha inawakamata na kuwafikisha mbele ya
vyombo vya sheria ili kuonesha kwamba kuna umuhimu wa mtu kufanya kazi.
Alisema kuwa kila kaya ni lazima iwe na mipango thabiti ya
kukabiliana na umaskini, hatua ambayo itasaidia kuinua hali zao za maisha
na sio kugeuka kuwa watazamaji au mabingwa wa kulalamika na
kuelekeza lawama zao kwa serikali.
Katika hatua nyingine, halmashauri ya wilaya ya Mbinga
kupitia idara ya kilimo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016
imefanikiwa kugawa mbegu za mbaazi kilo 8,000 kwa wakulima wa wilaya hiyo,
ambazo tayari zimeshapandwa katika msimu wa kilimo wa mwaka huu.
Pamoja na mambo mengine, Ofisa mazao wa wilaya hiyo
Deodatus Kisima alieleza kwamba lengo la mpango huo ni kuwasaidia wakulima
waweze kufanikisha malengo yao katika shughuli zao za kilimo, hatua
ambayo itawafanya wajiinue kiuchumi kutokana na kulima kwa njia ya kisasa
na kutumia mbegu bora zinazozaa vizuri, ili kuepusha hatari ya kutumia mbegu zisozofaa.
|
No comments:
Post a Comment