Tuesday, May 3, 2016

WAKULIMA WATAKA MFUKO WA VIDUNG'ATA UFUTWE

Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

WANACHAMA wa chama cha ushirika MBIFACU wilayani  Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameitaka Halmashauri ya wilaya hiyo kuufuta mfuko wa Vidung’ata ambao unahudumia wakulima wa zao la kahawa  wilayani humo, kwa kile walichodai kwamba mfuko huo umekuwa ukiwanufaisha baadhi ya watendaji waliopo serikalini na sio wakulima hao.

Aidha walieleza kuwa makato ya fedha wanazokatwa katika kila msimu wa mavuno ya kahawa ni makubwa mno, ambapo fedha hizo zililenga kwa ajili ya kununua madawa ya kuhudumia zao hilo lakini cha kushangaza dawa zinazonunuliwa mkulima husika hazimfikii ipasavyo.

Walisema kuwa lengo la kuunda mfuko wa Vidung’ata ni kwa ajili ya kudhibiti wadudu wanaoshambulia mti wa kahawa hasa katika kipindi cha masika na kwamba fedha wanazokatwa shilingi 50 kwa kila kilo moja ya kahawa mnadani Moshi ilipaswa zikafanye kazi iliyolengwa na sio vinginevyo.


Kauli hiyo ya wanachama hao wa MBIFACU wilayani Mbinga, ya kutaka mfuko huo ufutwe ilitolewa juzi kwenye mkutano wao mkuu uliofanyika mjini hapa na kueleza kuwa ni vyema waunde mfuko wa pembejeo za kilimo wao wenyewe na makato ya fedha zao, yaelekezwe huko na sio jambo hilo kushughulikiwa na watendaji wa serikali.

“Tunataka mfuko huu uondolewe kwenye mfumo wa serikali, upelekwe katika chama hiki cha ushirika lengo tuondokane na matatizo haya ya upatikanaji wa pembejeo za kuhudumia zao letu la kahawa kwa mkulima”, walisema.

Wilson Kapinga ambaye ni mkulima wa kutoka kata ya Ngima, alifafanua kuwa wamefikia hatua hiyo ya kuukataa mfuko huo kutokana na baadhi ya watendaji wa serikali ambao ni mabwana shamba kukosa uaminifu wa namna ya kufikisha madawa hayo kwa wakulima, ambapo huishia mikononi mwao kwa lengo la kujinufaisha wao binafsi.

Kapinga aliongeza kuwa maofisa ugani hao muda mwingi wamekuwa wanaishi mjini badala ya kuwa karibu na wakulima vijijini, ambapo kitendo hicho kinawafanya washindwe kuwajibika ipasavyo ikiwemo suala la kuwafundisha wakulima juu ya utunzaji bora wa mazao yao shambani.

Mkulima mwingine wa kahawa, Peter Komba kutoka kata ya Myangayanga wilayani hapa alibainisha kuwa umefika wakati sasa kwa watendaji hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu kutokana na kutowajibika ipasavyo katika maeneo yao ya kazi, ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho cha ushirika MBIFACU wilayani Mbinga, Stanley Lupogo aliunga mkono hoja hizo na kuongeza kuwa endapo wana malengo ya kuimarisha ushirika huo, wakulima wa kahawa hivi sasa wanapaswa kuzalisha zao hilo kwa wingi na ubora unaokubalika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo Lupogo alisisitiza kuwa endapo mkulima yeyote ataonekana kwa makusudi anataka kuharibu maendeleo ya chama hicho atachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

No comments: