Friday, May 20, 2016

MAAMBUKIZI VIRUSI VYA UKIMWI BADO NI TATIZO MKOA WA RUVUMA




Na Kassian Nyandindi,
Songea.

TANGU ilipoanzishwa Huduma ya Tiba na Matunzo (CTC) katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma mwaka 2004, kwa watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) hadi sasa watu 21,347 wamegundulika kuwa na ugonjwa huo, ambapo tayari watu 20,576 wamesajiliwa na kupewa huduma husika.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu.
Aidha kufuatia hali hiyo, Wadau wa afya katika Manispaa hiyo wamesikitishwa na hali mbaya ya maambukizi ya ugonjwa huo ambao hivi sasa unakua kwa kasi, huku watu waliopima VVU 213,212 kati yao 21,347 waligundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.

Hayo yalisemwa juzi na Mratibu wa ukimwi na kinga katika Manispaa ya Songea, Felista Kibena kwenye hafla fupi iliyoshirikisha wadau, wasambazaji na wauzaji wa bidhaa ya kondomu ambayo ilifanyika mjini hapa na kuandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la PSI Tanzania ikilenga pia kujadili juu ya usambazaji wa bidhaa hizo za afya.

Felista alifafanua kuwa Manispaa hiyo, imefanikiwa Kupunguza kiwango cha maambukizi toka asilimia 4.8 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 4 mwaka 2015 ambapo zaidi ya asilimia 60 wanatambua hali zao za maambukizi na kwamba kati ya hao waliosajiliwa ni wagonjwa 9,130 ambao wanatumia dawa za kupunguza makali ya VVU ikiwa ni sawa na asilimia 44.


Akizungumzia juu ya changamoto wanazokabiliana nazo katika utendaji wa kazi zao za kila siku, Mratibu huyo alisema kwamba bado wanakabiliwa na uhaba wa kondomu pamoja na upungufu wa vitendea kazi husika, hivyo wameweka mikakati ya kutuma maombi ya dharula kwenda bohari kuu ya dawa (MSD) ili waweze kupata vitendea kazi vya kutosha ikiwemo vifaa tiba vya kuweza kumaliza tatizo hilo.

Kwa upande wake Mratibu wa shirika la PSI  mkoa wa Ruvuma na Njombe, Wilfredy Mkungilwa alisema kuwa hali ya maambukizi  hayo ya virusi vya ukimwi katika Manispaa ya Songea inatisha kuliko mkoa wa Njombe, ambapo takwimu zilizotolewa hivi karibuni zinaonesha kuwa bado tatizo ni kubwa  na kwamba kuna kila sababu kwa serikali na wadau mbalimbali kushirikiana kwa kuchukua hatua ya kupunguza maambukizi hayo ikiwemo kuendelea kuelimisha jamii juu ya njia sahihi za kuzuia maambukizi mapya.

Alifafanua kuwa, shirika hilo ikiwa ni mdau mkubwa wa usambazaji wa kondomu ina lengo la kuikinga jamii dhidi ya hatari ya maambukizi mapya ya Ukimwi na magonjwa  ya zinaa, lakini kwa upande mwingine wafanyabiashara wanaweza kutumia fursa hiyo pia ya kuuza salama kondomu katika maduka yao ili huduma husika iweze kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.

Ofisa mauzo wa PSI mkoa wa Njombe na Ruvuma, Kinyumbi Kinyumbi aliongeza kuwa jumla ya kondomu 1,512,000 zimeuzwa  kwa mwezi January hadi Disemba mwaka jana kupitia wakala wa mkoa waliopo Songea, ambapo lengo lilikuwa kusambaza kondomu 5,279,904  ambapo katika mkoa wa Ruvuma walifanikiwa kusambaza kondomu  3,372,624.

Alifafanua kuwa baadhi ya wafanyabiashara  bado hawajajua umuhimu wa kuuza kondomu, kama bidhaa inayotakiwa kuwekwa na kuuzwa katika sehemu zao za biashara ambapo hali hiyo inasababishwa na imani zao za dini na mtazamo hasi huku wengine wakipuuza kufanya biashara hiyo.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa kondomu Michael Jackson, mjini Songea alipongeza shirika hilo kwa jitihada inazofanya na kuitaka serikali kuendelea kutoa elimu ya ukimwi kwa wananchi, ili kuweza kusaidia kupunguza maambukizi mapya na kizazi cha sasa kisiendelee kuangamia na ugonjwa huo.

Awali akihutubia kwenye ufunguzi wa hafla hiyo, Meya wa Manispaa ya Songea Abdul Shaweji alitoa msisitizo na kuagiza elimu dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo, iendelee kutolewa ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wa baa na nyumba za kulala wageni waweke kondomu kwenye maeneo yao.

Kadhalika Shaweji aliwataka wafanyabiashara  kuchangia juhudi za serikali katika kuhakikisha kwamba bidhaa bora za afya zinapatikana kwa urahisi na kwa wakati katika maduka yao ambayo yamesajiliwa kuuza bidhaa husika, ili jamii iweze kuondokana na maambukizi mapya ya ukimwi.

No comments: