Monday, May 23, 2016

WAPOTEZA MAISHA WAKATI WAKISAFIRI KUTOKA MBAMBA BAY KWENDA MALAWI KATIKA ZIWA NYASA

Ziwa Nyasa.


Na Kassian Nyandindi,
Songea.

WATU 11 wahofiwa kufa maji wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, kufuatia boti walilokuwa wakisafiria katika ziwa Nyasa wilayani humo kupoteza muelekeo na kuzama kwenye maji ya ziwa hilo, wakati wakielekea nchi jirani ya Malawi.

Aidha imeelezwa kuwa  tukio hilo lilitokea Mei 20 mwaka huu majira ya jioni, wakati watu hao wakitokea katika mji wa Mbamba bay kwenda Malawi wakiwa kwenye boti ndogo la mizigo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Zubery Mwombeji amethibitisha hayo na kueleza kuwa miili na majina ya watu hao bado haijapatikana na kwamba jitihada zinaendelea za kuitafuta, kwa kushirikiana na askari wa idara ya uhamiaji wilayani hapa.


Mwombeji alifafanua kuwa boti la serikali linalotumika kwa shughuli za uvuvi Halmashauri ya wilaya ya Nyasa, ndilo linalotumika kufanya msako mkali katika maeneo mbalimbali ya ziwa hilo kwa lengo la kuweza kupata miili ya marehemu hao.

Alibainisha kuwa ni siku mbili zimepita tokea boti hilo lizame maji kwenye ziwa hilo, ambapo taarifa rasmi za tukio hilo walizipata baada ya ndugu wa watu hao wanaohofiwa kufa maji kutoa taarifa, katika kituo kikuu cha Polisi Mbamba bay wilayani humo.

“Taarifa kamili tutatoa hapo baadaye na hayo majina ya wanaohofiwa kufa maji, lakini tukio hili kwa taarifa za awali tulizonazo limesababishwa na boti ndogo la mizigo walilokuwa wakisafiria, kuzidiwa na upepo mkali kutokana na hali ya ziwa hilo kuchafuka”, alisema Mwombeji.

Kamanda huyo wa Polisi aliongeza kuwa mpaka sasa mwelekeo wake haujulikani limezama wapi, hivyo kwa kushirikiana na serikali ya nchi ya Malawi na wilaya ya Nyasa Tanzania wanafanya jitihada ya kuendelea kutafuta miili na wapi boti hilo limezama ili waweze kutoa taarifa zilizokuwa sahihi hapo baadaye.

No comments: