Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WAKULIMA wa zao la Mhogo katika kijiji cha Kigonsera kata ya
Kigonsera wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali kuangalia uwezekano
wa kuwapatia mashine ya kusindika zao hilo na mazao mengine wanayolima,
ili waweze kuongeza thamani ya uzalishaji na kuwafanya waweze kupata soko la
uhakika la kuuzia mazao yao.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na wakulima hao, walipokuwa
wakizungumza na mwandishi wetu wakiwa kwenye shamba darasa la mhogo
linalotumika kwa ajili ya kufundishia wakulima kutoka maeneo mbalimbali
ya wilaya ya Mbinga na wakulima wa wilaya nyingine za mkoa huo, juu ya kilimo
bora cha mhogo.
Katibu wa kikundi cha Jitegemee, Oscar Ndunguru alisema kuwa wamekuwa
wakulima wazuri wa zao la mhogo na mazao mengine ya chakula na biashara
kutokana na elimu wanayoipata kutoka kwa maofisa ugani, ambapo changamoto kubwa
wanayokabiliana nayo sasa ni ya ukosefu wa mashine hiyo ya kusindika mazao
wanayozalisha, jambo ambalo linasababisha wakose soko la uhakika la kuuzia
mazao yao.
“Tumekuwa wakulima wazuri ambao tunafuata kanuni bora za
kilimo hiki cha mhogo, bado tatizo kubwa linalotukabili hapa kwetu ni ukosefu
wa soko la uhakika ambalo linachangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ukosefu wa
mashine ya kisasa ya kusindika zao hili, ili tuweze kuongeza thamani”, alisema Ndunguru.
Alisema kuwa, wakati umefika kwa serikali kupitia halmashauri
ya wilaya ya Mbinga, kuona umuhimu wa kuwasaidia wakulima hao kwa kuagiza
mashine nyingi za kusindika mazao mbalimbali yanayozalishwa wilayani humo, ili
kuweza kuwafanya wakulima waweze kuondokana na umaskini.
Naye mkulima aliyejitambulishwa kwa jina la Nuhu Kisoma, alieleza
kuwa wamekuwa pia wakizalisha mazao mengine ya chakula na biashara kama vile
alizeti, mhogo, mahindi na mbaazi.
Alisema kuwa endapo serikali itawathamini wakulima na
kuwaunga mkono katika shughuli zao kwa kuwanunulia mashine za usindikaji
mazao wilayani humo, wataweza kupiga hatua mbele badala ya kusubiri wateja
wachache ambao huwafuata mashambani mwao na kuwarubuni kuwauzia mazao yao, kwa
bei ndogo ambayo hailingani na gharama ya uzalishaji.
Kwa upande wake Meneja wa shirika la SIDO mkoa wa Ruvuma, Emmanuel
Makele aliwataka wakulima hao kuongeza jitihada katika uzalishaji wa mazao hayo
na kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali, ili serikali iweze kuwafikia kwa
urahisi katika utoaji wa huduma zake.
Makele alisema, kuna kila sababu kwa wananchi kutumia
fursa ya ardhi waliyonayo hapa nchini kwa kujikita zaidi katika shughuli
za kilimo badala ya kusubiri msaada kutoka serikalini, kwani tabia hiyo
inaweza kuchelewesha maendeleo yao na kutofikia malengo yaliyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment