Rais John Pombe Magufuli. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI imeombwa kuingilia kati na kutafuta ufumbuzi juu ya mgogoro
wa mashamba ambao unaendelea kufukuta katika kitongoji cha Ndiyomana kilichopo
kijiji cha Msinji kata ya Ligoma wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kati ya wakulima
na wageni wa kutoka shirika la WWF ambao hufanya uwekezaji wa utunzaji wa
misitu na ufugaji wa wanyama wilayani humo.
Mgogoro huo ambao umedumu kwa muda mrefu sasa na kufikia
hatua ya kuwa kero kwa wananchi wa kitongoji hicho, wamemwomba Rais John
Magufuli kuingilia kati na kuweka msimamo ambao utaweza kumaliza kero hiyo.
Wakulima zaidi ya 690 ndio wanaolalamikia juu ya hali hiyo
baada ya wageni wa hao kupora ardhi yao huku uongozi wa wilaya ya Tunduru licha
ya kupelekewa kero hiyo mezani, bado haijaona umuhimu wa kusikiliza kilio chao na
kuchukua hatua za haraka dhidi ya malalamiko ya wakulima hao.
Wakifafanua juu ya suala hilo, walisema mwaka 2015 kijiji cha
Msinji kilipokea wageni kutoka kwenye shirika hilo la WWF wenye lengo la kutaka
kuanzisha miradi katika hifadhi, lakini wananchi wa kijiji hicho hawakushirikishwa
jambo ambalo linawafanya wakose haki zao za msingi.
Pia walisema kutokana na uroho wa fedha na ubinafsi wa uongozi
wa kijiji hicho uliamua kuchukua maamuzi yao pekee yao, bila kuwashirikisha kwa
kugawa eneo la wakazi wa kitongoji cha Ndiyomana ili liweze kuwa eneo la
hifadhi, kitendo ambacho kimeelezwa kuwa ni cha unyanyasaji dhidi yao.
“Baada ya kubaini kitendo hiki ni cha unyanyasaji, tulichukua
hatua ya kufikisha kilio hiki katika ngazi ya wilaya ambapo kwa muda mrefu sasa
tumekuwa tukisubiri majibu hakuna mafanikio au utekelezaji wowote uliofanyika”,
walisema.
Miongoni mwa waliolalamikia hali hiyo na kumtaka Rais
Magufuli aingilie kati ni Seleman Sharif, Omar Juma, Jafari Mnuma na Athuman
Bilahi walisema kuwa endapo serikali haitachukua hatua za makusudi za kuutatua
mgogoro huo mapema, ipo hatari ya kuzuka kwa ugomvi kati yao na wawekezaji hao
wa WWF.
Walieleza kwamba wanaiomba serikali isikilize kilio chao
ambacho hivi sasa wameshindwa kupata suluhisho la kudumu, kutoka kwa uongozi wa
wilaya ya Tunduru.
Jitihada za kumpata Mkuu wa wilaya hiyo, Agnes Hokororo zilishindikana
kutokana na kuwa safarini kwa shughuli za kikazi ambapo mwandishi wetu
alifanikiwa kuongea na Ofisa tawala wa wilaya ya Tunduru, Ghaib Lingo ambaye
alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo huku akiahidi kuunda tume ya kushughulikia
swala hilo.
No comments:
Post a Comment