Na Steven Augustino,
Namtumbo.
WAZAZI wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, wameshauriwa
kupeleka watoto wao katika Chuo cha ualimu cha ushirika kilichopo wilayani
humo, ili waweze kupata elimu ambayo itawakomboa katika maisha yao, hatimaye wataweza
kuondokana na umaskini.
Mkuu wa chuo hicho, Wallfram Mpulo alisema hayo
katika mahafali ya kwanza ya wahitimu wa ualimu ngazi ya cheti daraja la tatu A,
tangu kilipoanzishwa mwezi Julai mwaka 2014 wilayani humo.
“Wazazi msiogope kuleta wazazi wenu katika chuo hiki, leteni
vijana wenu wasome hapa shuleni na waweze kujipatia elimu itakayowasaidia
katika maisha yao, chuo hiki kimesajiliwa na wizara husika na kinatambulika
kisheria”, alisema.
Mpulo alisema kuwa baada ya kuanzishwa kwa chuo hicho,
uongozi ulifuata taratibu na kufanikiwa kusajiliwa na Wizara ya
elimu na mafunzo ya ufundi na kupewa namba usajili CU 142 ya Juni
17/2014 na Septemba 8/2015 kilipata namba ya usajili wa mtihani
REG/TLF/128P chini ya Baraza la mtihani la Taifa (NACTE).
Alisema ameamua kuvunja ukimya huo, ili kuondoa dhana iliyojengeka
miongoni mwa wananchi wa wilaya hiyo kwamba chuo hakijasajiliwa jambo
ambalo sio la kweli na limekuwa likiwafanya vijana wa eneo la wilaya ya
Namtumbo, kuacha kujitokeza kuomba kusoma chuoni hapo na kufanya
vijana wengi wanaosoma hapo wanatoka maeneo ya mbali na wilaya hiyo.
Kufuatia hali hiyo aliwataka wananchi hao kuondoa dhana
hiyo potofu, na kwamba chuo hicho kimesheheni wakufunzi wazuri
na wazoefu wa kufundisha mambo kisheria kadiri ya taratibu za
wizara zinavyotaka.
Naye Mkurugenzi na mmiliki wa chuo hicho, Awadhi
alisema kuwa aliamua kutumia fedha yake ya pensheni
ya utumishi serikalini katika kuhakikisha anaanzisha
chuo hicho kwa lengo la kuhakikisha vijana wa Namtumbo,
wanapata fursa ya kusoma ualimu.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo Ofisa maendeleo
ya jamii wilaya ya Namtumbo Martin Mtani, ambaye alimwakilisha Mkuu wa
wilaya hiyo Chande Nalicho pamoja na mambo mengine alimpongeza
Mkurugenzi wa chuo hicho kwa kujitoa kukianzisha, kwa kutumia fedha yake ikiwa
ni lengo la kuendeleza taaluma katika jamii.
Kadhalika Mtani alitoa mwito kwa wananchi wa wilaya hiyo
na wilaya zingine hapa nchini, kutumia fursa hiyo iliyoletwa
na mwenyeji wa wilaya ya Namtumbo kujiunga katika chuo hicho ili waweze
kuendeleza vipaji vyao.
No comments:
Post a Comment