Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAANDISHI wa habari mkoani Ruvuma, wametakiwa kusaidia juhudi
zinazofanywa na Rais Dkt. John Magufuli katika kuwafichua watumishi wa umma ambao
wanajihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, ambavyo vinachangia kurudisha
nyuma kasi ya kuleta maendeleo kwa wananchi.
Yustina Chagaka. |
Aidha imeelezwa kuwa, vitendo hivyo vinavyofanywa na
watumishi hao hasa katika miradi ya maendeleo inakwamisha
malengo ya serikali katika kupunguza tatizo la umaskini kwa baadhi ya maeneo
hapa nchini, kwani miradi inayosimamiwa au kutekelezwa na wala rushwa inajengwa
chini ya kiwango na hivyo kushindwa kuleta tija iliyokusudiwa.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Mkuu wa Taaisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Ruvuma, Yustina Chagaka wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea.
Alisema kuwa vitendo vya rushwa, imekuwa ni kero kubwa katika
jamii hivyo kila mmoja anapaswa kuhakikisha anatoa ushirikiano wa kutosha kwa
taasisi hiyo, ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua ikiwemo kuwafikisha Mahakamani.
“Tumieni kalamu zenu kuwafichua watumishi wa umma, wanaojihusisha
na vitendo vya rushwa katika mkoa wetu, wao ndiyo kikwazo kikubwa cha kuongeza umaskini hapa
nchini, waandishi wa habari mnayo nafasi kubwa ya kuwabaini watu hawa”, alisema
Chagaka.
Kwa mujibu wa Chagaka aliongeza kuwa waandishi wa habari
wakitumia vizuri kalamu yao wana nguvu kubwa kuliko kitu chochote, kwani wanao uwezo
wa kumfikia kila mtu katika jamii na popote pale wanapoishi.
No comments:
Post a Comment