Na Steven Augustino,
Tunduru.
MAHAKAMA ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imemhukumu Ofisa
mthamini ardhi mstaafu wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Bernad Nyasi (60) kutumikia
kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia katika kosa la kughushi
nyaraka na kutoa hati za uongo, kwa wateja waliotakiwa kupewa vipande vya ardhi
wilayani humo.
Adhabu hiyo ambayo pia ilimpatia nafasi kwa kumtaka mtuhumiwa
huyo kulipa faini ya shilingi 500,000 ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya
wilaya hiyo, Gladys Barthy baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa katika
shauri hilo la jinai namba 6/2016.
Katika hukumu hiyo Mahakama hiyo, pia imewaachilia huru
washtakiwa wengine wawili waliokuwa wanakabiliwa na shtaka hilo ambapo
mpima ardhi wa Halmashauri hiyo, Mohamed Hamis (35) na mhudumu wa ofisi ya
ardhi ya wilaya ya Tunduru Masud Kanduru (40).
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka hayo, Mahakama hiyo ilimkuta
na hatia Ofisa ardhi huyo katika shtaka la nane kati ya makosa 10 yaliyokuwa yanawakabili
watuhumiwa hao ambalo ni la kughushi hati namba TUR/77 ya Mei 20 mwaka 2015
iliyokuwa ikimtambulisha Mariam Nyenje kuwa ni mmiliki halali wa kiwanja namba
104 Ploti namba 0 katika eneo la Nakayaya wilayani hapa.
Akiwasomea mashitaka hayo Mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi
wa Polisi Inspekta Songelael Jwagu, alisema kuwa pamoja kwamba watuhumiwa hao
walifanya kosa la kughushi nyaraka mbalimbali kinyume cha sheria namba 333 na
335 (a) na 337 vya sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16, kama ilivyofanyiwa
marekebisho mwaka 2002.
Katika mashtaka hayo pia watuhumiwa hao, walidaiwa kutenda
kosa la kuwasilisha hati za uongo kwa wateja wao kinyume cha sheria namba 342
cha kanuni ya adhabu sura ya 16.
Inspekta Jwagu alisema mnamo Julai Mosi mwaka 2013 watuhumiwa
hao walighushi barua yenye kumbukumbu namba TUR/ 7914 ikiwa inamtaja Maembe
Sabule Wambura, kuwa ndiyo mmiliki halali wa kiwanja namba 152, kitalu FF
kilichopo katika mtaa wa Nakayaya mjini hapa.
Aliwataja wengine ambao walitapeliwa kwa mtindo huo kuwa ni,
Rashid Athuman Issa aliyeandikiwa hati namba TUR/8811/Q ya Disemba 7 mwaka 2014
ikiwa inamtambulisha kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa kiwanja namba 190,
kitalu namba Q kilichopo katika eneo hilo la Nakayaya.
Pia katika hati hiyo alilitaja shtaka jingine, lililokuwa
linawakabili watuhumiwa hao kuwa ni shauri la kughushi barua yenye kumbukumbu
namba Tu/9080 /1/BSR ya Julai 1 mwaka 2013 ikiwa inaonesha kwamba iliandikwa na
Ofisa ardhi wa wilaya hiyo, Nyasi ikimpatia idhini Peter Rioba Mnanka kuwa
ndiyo mmiliki halali wa kiwanja namba 53 kitalu 0 kilichopo kwenye eneo la
Nakayaya Tunduru mjini.
No comments:
Post a Comment