Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya wananchi wanaoishi katika kijiji cha Ntunduaro kata
ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamempongeza Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya hiyo Venance Mwamengo kwa kuchukua hatua ya kufunga
mashine ya kukusanyia ushuru katika eneo la Amani Makolo, ambalo husafirishwa
mkaa wa mawe kwenda nje ya wilaya hiyo kitendo ambacho kwa kiasi kikubwa
kimesaidia kudhibiti mapato ya fedha yatokanayo na mkaa huo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Walisema kuwa hapo awali kabla ya kufungwa kwa mashine hiyo
ya Electronic (EFD’S) mapato mengi yalikuwa yakipotea kutokana na kukusanywa
kwa njia ya vitabu vya risiti, ambapo watendaji waliokuwa wakipewa dhamana ya
ukusanyaji wa fedha hizo za ushuru walikuwa hawawajibiki ipasavyo.
Theodosia Mahundi mkazi wa kijiji hicho aliwaeleza waandishi
wa habari kuwa udhibiti huo wa mapato unapaswa kufanywa kwa kutumia mashine
hiyo, katika kila eneo ambalo serikali inakusanya mapato ili kuweza kudhibiti
mianya ya wajanja wachache, ambao wamekuwa wakitafuta njia za ufujaji wa fedha
za serikali.
Mahundi alisema kuwa ni faraja kwao kuona mapato hayo jinsi
yanavyodhibitiwa na kwamba wanaimani kuwa hata serikali, itaweza kuwahudumia
wananchi wake kwa kuwapelekea huduma muhimu kama vile madawa kwenye zahanati na
vituo vya afya kwa wakati.
Naye Renatus Mapunda mkazi wa kijiji cha Amani Makolo kata ya
Amani Makolo alisema kuwa hapo awali madereva wengi wanaosafirisha mkaa wa mawe
kwenda nje ya wilaya hiyo, ameshuhudia wakiwa wanakwepa kulipa ushuru huo
ambapo alitoa ushauri kwa kuitaka serikali kuendelea kuongeza nguvu ya udhibiti
wa mapato yatokanayo na mkaa huo, ili jamii iweze kunufaika nayo kwa njia ya
kuwaletea maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake Ofisa anayedhibiti mapato yatokanayo na
ushuru wa mkaa wa mawe wilaya ya Mbinga, Justine Ambrose alieleza kuwa mashine
hiyo ya EFD’S ilifungwa katika eneo hilo Februari 24 mwaka huu kwa lengo la
kuleta ufanisi wa kazi husika.
Ambrose alibainisha kuwa hivi sasa ukusanyaji wake umekuwa
mzuri ambapo kila gari linalosafirisha mkaa hutozwa shilingi 30,000 na kwamba
kwa siku zaidi ya magari 30 yamekuwa yakilipa ushuru.
“Hapo awali madereva hawa wanaosafirisha mkaa huu wa mawe
walikuwa wakitunyanyasa kwa kututolea lugha chafu, wakati mwingine walikuwa
wakikimbia kwa lengo la kutaka wasilipe ushuru lakini tumeweza kufanya jitihada
ya kuwadhibiti kikamilifu”, alisema Ambrose.
Hata hivyo aliishauri serikali kuweka utaratibu kwa kuwatoza
faini madereva wanaokwepa kulipa ushuru pale wanapokamatwa, ili iweze kuwa
fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment