Tuesday, February 7, 2017

SONGEA WAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 26.5

Na Kassian Nyandindi,    
Songea.

BARAZA la Madiwani katika Halmashauri ya wilaya ya Songea mkoani Ruvuma limepitisha bajeti ya shilingi bilioni 26,531,667,816 katika mwaka wa fedha wa 2017 hadi 2018 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi wilayani humo.

Bajeti hiyo ilipitishwa juzi kwenye kikao maalumu cha Baraza hilo ambacho kilikuwa kikiongozwa Mwenyekiti wake, Rajab Mtiula katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo ambacho kilihudhuriwa na wakuu wa idara pamoja na watendaji wa kata wa wilaya hiyo.

Akiwasilisha bajeti ya mpango wa maendeleo kwa mwaka huo wa fedha mbele ya baraza la madiwani hao, Afisa mipango wa halmashauri hiyo Shaban Millao alisema kuwa bajeti hiyo imezingatia makubaliano waliyoketi katika vikao vya kamati mbalimbali.


Millao alisema kuwa vipaumbele vya bajeti hiyo kwa mwaka 2017/2018 ni kukamilisha miradi ya miaka ya nyuma ambayo ilikuwa bado haijakamilika ujenzi wake, kuajiri watumishi ili kuweza kujaza nafasi wazi zilizopo 398 wakiwemo wakuu wa idara ya maji, mifugo na uvuvi, ujenzi, kilimo, umwagiliaji, ushirika na afya.

Aliongeza kuwa bajeti hiyo pia imelenga kuboresha na kuendeleza usafi wa mazingira, kupambana na tatizo la utapiamlo, ujenzi wa miundombinu ya elimu katika shule za msingi na sekondari, kuboresha huduma za afya kwa kukamilisha ujenzi wa zahanati sita, kutengeneza madawati na viti kwa ajili ya shule za msingi na sekondari, ujenzi wa nyumba za watumishi katika shule za msingi na sekondari, kuboresha mtandao wa barabara za halmashauri, ujenzi wa nyumba za watumishi na wakuu wa idara pamoja na kuandaa mpango mkakati mpya wa maendeleo ya halmashauri hiyo.

Afisa mipango huyo alisema kuwa bajeti ya halmashauri pia imepungua kutoka ukomo wa bajeti wa shilingi bilioni 31,130,532,510 kwa mwaka 2016/2017 na kuwa shilingi bilioni 26,531,667,816 kwa mwaka 2017/2018 ikiwa sawa na upungufu wa asilimia 17 ambapo amedai kuwa upungufu huo umetokana na ukomo wa bajeti ya mishahara kutokana na mwaka huo mishahara ilikuwa pamoja na halmashauri ya wilaya Madaba kabla ya kutengana.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Songea, Rajab Mtiula amewapongeza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Simon Bulenganija, Afisa mipango Shaban Millao pamoja na timu nzima ya wataalamu kwa kuandaa vizuri taarifa ya bajeti na mpango wa maendeleo ya wananchi, kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambapo amedai kuwa endapo itapitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaweza kuleta sura nzuri ya mafanikio makubwa kwenye  upande wa miradi ya maendeleo.

No comments: