Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WALIMU wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya
wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi zao
ikiwemo kuacha vitendo vya ulevi na utoro kazini.
Aidha wamesisitizwa kuwahi na kuwa katika mazingira ya kazi
wakati wote na kufuata taratibu za kazi zao kwa mujibu wa nafasi walizonazo
kazini.
Gombo Samandito. |
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya
wilaya hiyo, Gombo Samandito wakati alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha
tathimini ya maendeleo ya elimu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa Katoliki
Jimbo la Mbinga mjini hapa.
“Walimu mnatabia ya kuwa watoro kazini natambua mnajua kwamba
zikipita siku tano haupo kazini nakufukuza kazi, wakati wa kazi fanyeni kazi zenu
kwa kutekeleza ipasavyo majukumu mliyopewa mkayasimamie haya vizuri msiwe
sehemu ya matatizo”, alisisitiza Samandito.
Samandito alisisitiza pia kwa atakayepuuza maagizo yake hatua
kali za kinidhamu zitachukuliwa dhidi yake ikiwemo kufukuzwa kazi huku
akiongeza kuwa adui mkubwa wa maendeleo katika maisha ya kila siku ya binadamu
ni tabia ya mtu husika hivyo walimu hao wanapaswa kujiangalia kwanza wenyewe na
kubadilika mara moja kuwa na tabia nzuri kazini.
Vilevile amekemea tabia ya walimu kukopa hovyo kwenye taasisi
za kifedha kupita kiasi jambo ambalo alieleza kuwa ni kinyume na taratibu
husika, hivyo wakope kwa kufuata taratibu zilizowekwa na sio vinginevyo.
“Walimu jaribuni kuliangalia hili haya mambo yaangalieni sana
ole wake nitakayemkamata atakiona cha mtemakuni, hiyo huruma ya msamaha sina
kabisa nitakuchukulia hatua za kinidhamu pale nitakapokuona umekiuka maagizo
haya ikiwemo kukufukuza kazi”, alisisitiza.
Kwa upande wao wakichangia hoja katika kikao hicho cha Wadau
wa elimu kwa nyakati tofauti, Magnus Mpokwa ambaye ni mzee maarufu kutoka kata
ya Mkako wilayani Mbinga alisema kuwa maofisa elimu kutoka ngazi ya kata hadi
wilaya wanapaswa sasa kuacha kukaa maofisini badala yake waondoke na kwenda
vijijini kukagua maendeleo kwa shule za msingi na sekondari.
Hata hivyo naye Mario Kitusi ambaye ni mwalimu Mkuu shule ya
msingi Mahumbato wilayani humo alisisitiza kuwa ili elimu iende vizuri ni
lazima kuwepo na mshikamano kati ya wazazi, walimu na viongozi wengine wote na
kwamba serikali inapaswa pia kuboresha maslahi ya elimu ili taaluma iweze
kusonga mbele.
No comments:
Post a Comment