Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
SERIKALI hapa nchini imezuia shughuli za uchimbaji wa madini
ya vito katika mto Muhuwesi wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, hadi hapo taarifa
za kitaalamu zitakapotolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la tathimini na
ukaguzi husika.
Agizo hilo la kuzuia kazi hiyo kufanyika katika mto huo limetolewa
hivi karibuni wilayani humo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
alipofanya ziara yake kwenye mto huo ili kujionea hali ya eneo hilo kufuatia
ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kanje Ally na
majeruhi mmoja ambao waliingia na kuanza kuchimba ndani ya mto huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa madini mkazi wa wilaya ya Tunduru,
Mhandisi Fredrick Mwanjisi alisema kuwa zaidi ya watu sita walivamia eneo hilo
la mto kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kinyume cha taratibu, kutokana
na kutokuwa na vibali vilivyowaruhusu kufanya shughuli hiyo ya uchimbaji katika
eneo hilo.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba shughuli za uchimbaji wa madini hayo
ndani ya mto Muhuwesi zilisimamishwa tangu mwaka 2014 kufuatia pingamizi kutoka
kwa Mamlaka ya bonde la mto Ruvuma na bonde la Kusini, kwa kuzingatia sheria ya
usimamizi wa rasilimali za maji namba 11 ya mwaka 2009 na sheria ya usimamizi
wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004.
Kufuatia taarifa hiyo na baada ya kujionea hali halisi na
kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo pamoja na viongozi wao, Waziri Muhongo
aliagiza kusitisha haraka shughuli zote za uchimbaji madini kwenye mto huo hadi
hapo taarifa ya tathimini ya athari ya shughuli ya uchimbaji kwa mazingira ya mto
Muhuwesi itakapokamilika na kuwasilishwa na wataalamu kutoka Mamlaka ya bonde
la mto Ruvuma, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na
Wizara ya Nishati na Madini (MEM).
Ili kuhakikisha suala hilo linapata ufumbuzi wa haraka,
Waziri Muhongo alitoa miezi mitatu kwa wataalamu husika kutoka mamlaka hizo
wawe wamewasilisha taarifa hiyo kwake na kwa uongozi wa wilaya ya Tunduru
tayari kwa kuanza kufanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment