Martin Mbawala, ambaye ni Mratibu wa mafunzo ya sheria ya watu wenye ulemavu wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma akiwasisitiza jambo washiriki wa mafunzo hayo katika kata ya Mpepai wilayani hapa. |
Mbinga.
BAADHI ya Watu
wenye ulemavu wanaoishi katika kata ya Mpepai Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoa
wa Ruvuma, wameiomba serikali izingatie suala la uboreshaji wa miundombinu
rafiki kwa watu wenye ulemavu hasa kwenye majengo ya umma yanayoendelea
kujengwa hapa nchini kwa ajili ya kutolea huduma mbalimbali.
Washiriki wa mafunzo. |
Vilevile
wamesisitiza jamii kuacha tabia ya kuwafungia ndani watoto wenye ulemavu na
kwamba wametakiwa kujenga mazoea ya kuwafichua watu wenye tabia ya kuwaficha
watoto hao, ili wahusika wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria
ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
Hayo
yalisemwa juzi na Walemavu hao kwa nyakati tofauti wakati walipokuwa
wakichangia hoja mbalimbali katika mafunzo ya siku mbili ya sheria ya watu
wenye ulemavu, yaliyofanyika katika kata ya Mpepai halmashauri ya mji huo ambayo
yalifadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Foundation for Civil
Society.
Akichangia
hoja kwenye mafunzo hayo Felix Ndomba mkazi wa kata hiyo alisema kuwa jamii
inapaswa pia kuacha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu ikiwemo
unyanyasaji, ubaguzi badala yake wanapaswa kujenga mazoea ya kuwapenda,
kuwajali na kuwahudumia ipasavyo kama walivyokuwa watu wengine ambao hawana
ulemavu.
“Ndugu zangu
tunapaswa kuwa wasikilizaji wazuri katika mafunzo haya huko tuendako
tukayatumie vyema kwa kufikisha ujumbe huu pia kwa wenzetu ambao hawakubahatika
kuhudhuria hapa ili waweze kutambua haki zao za msingi”, alisisitiza Ndomba.
Naye Amos
Komba ambaye ni Hakimu wa Mahakama ya mwanzo wilaya ya Mbinga akitoa mada
katika mafunzo hayo, alisisitiza pia mlemavu yeyote yule anatafsiriwa kuwa ni
binadamu mwenye haki sawa kama walivyokuwa watu wengine ambao hawana ulemavu
hivyo anastahili kupata haki zote za msingi kama watu wengine na sio vinginevyo.
Komba alisema
kuwa pale mtu mwenye ulemavu anaponyanyaswa kwa namna moja au nyingine, mtu
yeyote sheria inamruhusu kutoa malalamiko kwa kamati husika ya maofisa wa
ustawi wa jamii au kwenda kushtaki Mahakamani kufungua mashtaka dhidi ya kosa
aliloliona linafanyika.
“Kila
binadamu amezaliwa hapa duniani kwa ajili ya kuishi kwa hiyo tunapaswa
kuthamini utu wa kila mtu, tunapaswa kutambua kwamba mlemavu ni sawa kama
alivyokuwa mtu mwingine ambaye hana ulemavu hivyo hatupaswi kuwatenga au
kuwabagua”, alisisitiza Komba.
Pia Komba
aliongeza kuwa wajibu wa Wizara za serikali hususan kwa ile inayoshughulikia
mambo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali inapaswa kuhakikisha kwamba, inajumuisha
taarifa za miradi inayotekelezwa na wizara hiyo itakayogusa huduma mbalimbali
zinazokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu, waandishi, wasanifu majengo na watu
wengine wanaojihusisha na ujenzi huo wahakikishe kwamba majengo mapya na
viwanja vya michezo vinabadilishwa ili kuwawezesha walemavu wanaingia na kutoka
bila kizuizi.
No comments:
Post a Comment