SIKU zote jamii imekuwa ikitambua kwamba ardhi ni rasilimali
muhimu katika kujiletea maendeleo kwa kuitumia kuendeshea shughuli mbalimbali
ikiwemo kilimo, ujenzi wa makazi, ufugaji na shughuli nyingine ambapo kutokana
na umuhimu wake baadhi ya viongozi kwenye vitongoji na vijiji wamekuwa
wakitumia umuhimu wa mahitaji ya ardhi kujinufaisha kwa kuigawa bila kuzingatia
sheria, sera na kanuni zilizopo za ugawaji ardhi.
Kutokana na uwepo wa hali hiyo, sasa imekuwa ikisababisha hata
kuibuka kwa migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo hapa nchini na haya yote
yanasababishwa na viongozi hao kutaka kuingia madarakani kwa kujinufaisha
matumbo yao.
Miaka ya 1990 serikali ya Tanzania ilijihusisha katika
mchakato wa kutengeneza sera na mfumo wa sheria ambayo ilipelekea uundaji wa
sera ya Taifa ya ardhi ya mwaka 1995 na kutungwa kwa sheria ya ardhi ya mwaka
1999 ambazo ni sheria ya ardhi ya vijiji namba tano ya mwaka 1999 na sheria ya
ardhi namba nne ya mwaka 1999 ambapo hizo zote, zimekuwa zikieleza mpango wa
matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji lakini licha ya kuwepo kwa sheria hizo
bado changamoto ya migogoro ya ardhi imekuwa ikiendelea kujitokeza katika
baadhi ya maeneo.
Aidha juhudi hizo bado zinahitajika katika kukuza
uelewa wa wanakijiji juu ya mifumo ya kisheria katika masuala ya haki za ardhi,
uwezo wa uwekezaji mkubwa wa kilimo na uhusiano na ustawi wa wakulima wadogo,
kilimo endelevu na maendeleo endelevu ya nchi kwa ujumla.
Hivyo katika kuliona hilo kuwa na umuhimu huo wa kipekee, Halmashauri
ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imeweza kuwaelimisha wananchi wake wilayani
humo juu ya masuala ya upimaji wa ardhi yao ikiwemo viwanja, mashamba na miji
midogo ili kuweza kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.
Gombo Samandito akiwa ameshika moja kati ya Hati ya hakimiliki ya kimila. |
Migogoro hiyo ya ardhi mingi imekuwa ikijitokeza baina ya
wakulima na wafugaji, wakulima na wawekezaji, mtu kwa mtu na kijiji kwa kijiji
ambayo wakati mwingine imekuwa ikisababisha watu kupoteza maisha, kupata
ulemavu na upotevu wa hata mali zao.
Wengi tumekuwa tukishuhudia kwamba kushamiri kwa migogoro
hiyo imekuwa pia ikisababisha kudumaa kwa uchumi wa wananchi kwani wakati
mwingine wakulima wamekuwa wakishindwa kuzalisha mazao, wafugaji mifugo yao
kujeruhiwa, wawekezaji nao mali zao kuharibiwa na wananchi kutokana na kugombea
ardhi kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo kilimo, makazi
na ufugaji.
Mwandishi wa Makala haya amefanya mahojiano na Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Gombo Samandito ambaye ameeleza kwamba
hadi kufikia sasa mashamba yenye zaidi ya ukubwa wa ekari 78,149.065 sawa na
hekta 31,259.626 yameingizwa na kupimwa katika mpango wa upimaji ardhi wa
wilaya hiyo.
Samandito anasema kuwa halmashauri hiyo inaendelea kutekeleza
sheria za ardhi pamoja na kutimiza agizo la serikali la kupima kila kipande cha
ardhi na kukimilikisha kwa walengwa husika, huku ikiendelea kuhamasisha
wamiliki wa viwanja na mashamba kulipia kodi za ardhi pamoja na kuviendeleza
viwanja vyao kwa mujibu wa sheria, ikiwa pamoja na kusambaza hati za madai ya
kodi kwa wadaiwa sugu na wale wanaoshindwa kulipa hufikishwa Mahakamani.
Anabainisha kuwa jumla ya hati ya hakimiliki za kimila 20,000
zinatarajiwa kutolewa kwa wananchi wa vijiji 121 vilivyopo katika kata 29 za halmashauri
hiyo na kwamba mpaka sasa zaidi ya hati ya hakimiliki za kimila 3,000 zipo
tayari na wananchi wanatakiwa kukabidhiwa kwa utaratibu husika ulioandaliwa.
“Lengo kubwa hapa la kufanya hivi ni kuepuka migogoro ya
ardhi katika upangaji, upimaji na ugawaji wa viwanja baina ya wamiliki wa ardhi
na serikali yetu hivyo mpaka sasa tumeweza kupima ekari 70,000 hapa wilayani
kwa kutumia utaratibu wa upimaji shirikishi, bila kulipa fidia ambapo mmiliki
wa ardhi huchangia gharama ya upimaji kwa kutoa asilimia 40 ya viwanja
vitakavyopatikana katika ardhi yake,
“Utoaji wa asilimia hii ya viwanja huenda kwa halmashauri kwa
lengo la kufidia maeneo yote yatakayoangukia kwenye maeneo ya huduma za kijamii
kama vile barabara, maeneo ya wazi, ujenzi wa zahanati, masoko na shule huku
asilimia 60 ya viwanja itakayopatikana katika ardhi husika hubaki kwa mmiliki
wa ardhi na zoezi hili litaendelea kuwa endelevu kwa manufaa ya wananchi wetu”,
anasema Samandito.
Pamoja na mambo
mengine kwa upande wa utatuzi wa migogoro mbalimbali ya ardhi wilaya ya Mbinga,
imekuwa ikiendelea kupambana na utatuzi wa migogoro hiyo kwa kutenga siku moja
ya Ijumaa ya kila mwisho wa mwezi na kuanzisha dawati la kupokea kero za
wananchi zinazohusiana na masuala ya ardhi ili yaweze kutatuliwa.
Awali Samandito akizungumzia kabla ya zoezi hilo la upimaji
kuanza wilayani hapa, anafafanua kuwa miongoni mwa watu waliopatiwa mafunzo juu
ya manufaa ya zoezi hilo wakiwemo watumishi wa serikali watendaji kata na
vijiji, maafisa ugani, fundi sanifu ramani ambao baadaye walipita vijijini
kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wake wa kutekeleza zoezi hilo kabla
upimaji huo haujaanza.
Mafunzo hayo yalihusisha haki za ardhi kwa makundi
mbalimbali, sera na sheria zinazosimamia ardhi, mpango wa matumizi ya ardhi
vijijini, utatuzi wa migogoro ya ardhi ambayo yalilenga hasa kuwajengea uelewa
wananchi katika masuala ya haki za ardhi na kuwajengea uwezo zaidi katika
kuisimamia serikali katika usimamizi wa ardhi na rasilimali za nchi.
Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya wilaya hiyo anaongeza kuwa
wananchi wengi ni wakulima na wafugaji na kwamba shughuli zao kubwa zinahitaji
ardhi kwa ajili ya kuendesha shughuli hizo hivyo mara nyingi wamekuwa wakiingia
kwenye migogoro kutokana na uwepo wa mwingiliano usiokuwa na tija kwao baina ya
pande hizo mbili.
Anasisitiza kuwa umefika wakati sasa viongozi wa vijiji
waliopata elimu hiyo watumie nafasi yao katika kutatua changamoto ya migogoro
ya ardhi kwenye maeneo yao kwa kuwasisitiza wananchi wapime ardhi zao ili baadaye
waweze kuzimiliki kisheria na kuwa na hati ya hakimiliki ya kimila ambazo zitaweza
kuzuia na kuondoa chanzo cha kushamiri kwa migogoro ya ardhi isiyokuwa ya
lazima kwenye maeneo yao.
Anasema pia tatizo la wanaume kuwadharau wanawake kumiliki
ardhi kwenye ardhi za ukoo kwa kuwaona kuwa wanawake hawana haki ya kumiliki
ardhi kisheria licha ya sheria kueleza wazi kuwa mwanamke naye ana haki ya
kumiliki ardhi sawa na mwanaume, hivyo anaomba jamii iondokane na dhana hii
potofu na mtizamo huu hafifu uliopo katika jamii kulingana na mila na desturi
kwa kuona kwamba mwanamke hana haki ya kumiliki mali hususani kwenye ardhi sawa
kama ilivyo kwa wanaume.
Kadhalika Mratibu wa zoezi la upimaji ardhi wilayani humo,
Faraja Kaluwa anaeleza kwamba baadhi ya viongozi kutojua majukumu yao kama
viongozi katika kuongoza wananchi huko vijijini, hali hiyo nayo huchangia
viongozi hao kutotambua wajibu wao na mipaka yao ya kiutendaji ambapo kufanya
hivyo wamekuwa wakisababisha hata baadhi yao kugawa ardhi bila kuzingatia
sheria.
Pamoja na mambo mengine Kaluwa anabainisha kuwa ardhi inayotolewa
na kijiji haizidi ekari 50 na kwamba zaidi ya kiwango hicho muombaji anapaswa
kwenda ngazi ya halmashauri lakini baadhi ya viongozi kwenye vitongoji au
vijiji, kutokana na baadhi yao kuwa na uelewa mdogo hufanya hivyo kwa tamaa na
kutoa ardhi zaidi ya ekari 50 kwa muombaji jambo ambalo ni kosa kwa mujibu wa
sheria za nchi.
“Pia kuna tatizo wananchi kutokuwa na elimu katika suala zima
la matumizi bora ya ardhi hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika kutoa
elimu kwa viongozi kwenye vijiji, vitongoji na jamii kwa ujumla na uwepo wa
mawasiliano katika sekta za serikali katika kupanga mipango ya matumizi bora ya
ardhi ili kuweza kushirikiana katika utekelezaji wa shughuli za kupanga mipango
hiyo”, anasisitiza Kaluwa.
Hata hivyo kwa ujumla zoezi la upimaji ardhi kwa halmashauri
ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma, wananchi wengi wamelipokea kwa mikono miwili
baada ya kubaini kwamba litawaletea manufaa makubwa ya kukuza uchumi wao mara
baada ya kuanza kupata hati za hakimiliki ya kimila ambazo huwawezesha sasa hata kwenda
benki kukopa fedha za kufanyia shughuli zao za kimaendeleo, ikiwemo kuboresha
mashamba yao ya kahawa na mazao mengine mbalimbali ili waweze kuzalisha kwa
wingi na hatimaye kuondokana na umaskini.
No comments:
Post a Comment