Sunday, March 5, 2017

NAMTUMBO WALIA NA TATIZO LA UPUNGUFU WA DAWA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA

Na Yeremias Ngerangera,      
Namtumbo.

KUFUATIA kuwepo kwa tatizo kubwa la upungufu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma ya afya wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, Mbunge wa Jimbo la Namtumbo mkoani humo, Injinia Edwin Ngonyani amesikitishwa na hali hiyo na kuwaahidi wananchi wake kwamba tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili lisiendelee kuumiza wananchi.

Ngonyani ambaye pia ni Naibu  Waziri  wa  ujenzi, uchukuzi  na mawasiliano alipokea malalamiko hayo juzi kutoka kwa wananchi wake kwamba vituo vya afya vilivyopo katika Jimbo hilo imekuwa ni kero kubwa juu ya upatikanaji wa dawa pamoja na huduma zingine muhimu za matibabu.

“Hapa katika jimbo letu kero kubwa pia huduma za bima ya afya pia ni tatizo, maji pamoja na upungufu wa waganga katika vituo vya kutolea huduma ya afya tunaiomba serikali itatue tatizo hili”, walisema.


Akijibu juu ya kero hizo Mbunge huyo alisema kuwa kutokana na malalamiko hayo kuwa makubwa aliwaahidi wananchi wake wa Jimbo hilo kwamba, atazichukua kero hizo na kuzifikisha mahali husika ili ziweze kufanyiwa kazi hatimaye wananchi waweze kupata huduma na kuondokana na malalamiko hayo.

Agrey Mwansasu ambaye ni Kaimu Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, alikiri kuwepo kwa mapungufu ya dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya wilayani humo huku akiongeza kuwa hali hiyo inatokana na makundi matatu yaliyopewa msamaha na serikali kutibiwa bure.

Aliyataja makundi hayo kuwa ni wazee, watoto chini ya miaka mitano, akina mama wajawazito ambapo mara nyingi wanapoletwa kwa ajili ya matibabu katika vituo hivyo au zahanati mahali ilipo, hutumia dawa za wagonjwa wengine hatimaye husababisha upungufu wa dawa na kuzua malalamiko hayo yaliyopo sasa.  

No comments: