Sunday, March 12, 2017

KAMPUNI YA OVANS YAPONGEZWA KWA KUUNGA MKONO JITIHADA ZINAZOFANYWA NA SERIKALI

Mitambo ya Kampuni ya Ovans Construction Limited,  ikiendelea na kazi ya ujenzi uwanja wa michezo shule ya msingi Kiwanjani uliopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma.
Na Kassian Nyandindi,       
Mbinga.

KATIKA kuhakikisha kwamba jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano hapa nchini zinaendelea kuungwa mkono, Kampuni ya Ovans Construction Limited iliyopo wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma imejitokeza na kutoa mchango wake wa kukarabati uwanja wa michezo wa shule ya msingi Kiwanjani uliopo mjini hapa kwa manufaa ya jamii.

Aidha imefafanuliwa kuwa lengo la kuukarabati uwanja huo ni kuufanya uweze kuwa wa kisasa zaidi ambapo utaendana na zoezi la uoteshaji nyasi kwa mfumo wa kisasa, ili wanafunzi wa shule hiyo na vijana wa kutoka Mbinga mjini waweze kucheza mpira wa miguu na kufanya mazoezi mbalimbali ya viungo vya mwili.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Vallence Urio akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake amesema kuwa kampuni yake imetoa mchango wa vifaa kama vile Caterpiller, Roller, Dumper truck na Exacavator ambavyo vinatumika kwa ajili ya kuchimba udongo na kusawazisha uwanja huo.

Vallence aliongeza kuwa baada ya kumaliza kusawazisha pia wataushindilia vizuri na kuupanda nyasi ambazo zitapandwa kitaalamu na kwamba zikisha kua na kufikia kiwango bora kinachofaa zitakatwa kwa mashine maalumu tayari kwa uwanja huo kuuweka katika maandalizi ya kuanza kutumika kucheza michezo mbalimbali.


“Gharama ya mitambo yangu inayofanya kazi ya kuukarabati uwanja huu jumla yake ni shilingi milioni 16.4 tunafanya mambo yote haya ili kuweza kuimarisha afya za watu kwa kupenda kufanya mazoezi na hili pia ninaunga mkono, juhudi za serikali ya awamu ya tano kupitia Makamu wetu wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye huwataka Watanzania kuwa na mazoea ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha viungo vya miili yao”, alisema Vallence.

Vilevile ameeleza kuwa uwanja watautengeneza kwa mfumo wa kutaka watu wote waliopo katika mji wa Mbinga waweze kucheza michezo na kufanya mazoezi na kwamba nyasi hizo zitapandwa kitaalamu kwa muda wa siku tatu, baada ya kumwagwa mbolea aina ya Minjingu au DAP ili ziweze kukua vizuri na mpaka  kufikia mwishoni mwa mwezi wa nne mwaka huu zitakuwa zimeota vizuri na kukamilika matengenezo yake.

Naye Katibu wa timu ya soka ya vijana Mbinga Veteran FC Emmanuel Malila amemweleza mwandishi wetu kuwa, baada ya kuona mji wa Mbinga una uhaba wa viwanja vya michezo uongozi husika ulikaa na kujadiliana ni wapi wanaweza kuwa na uwanja wa kufanyia mazoezi kutokana na uwanja uliopo wa michezo unaomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliopo mjini hapa kuwa na mwingiliano wa matumizi mbalimbali.

“Kumekuwa na mwingiliano wa matumizi makubwa ya uwanja huu wa CCM ambao timu nyingi tumekuwa tukiutumia hadi sasa, ndipo tulipoliona hili tuliamua kwenye vikao vyetu kukaa na kamati ya shule ya msingi Kiwanjani tukakubaliana vizuri juu ya ukarabati huu unaofanyika hapa ambapo tunamshukuru Mwenyekiti wa kamati ya shule hii, Deo Ndunguru na wajumbe wake wa kamati kutukubalia ombi letu la kuutengeneza uwanja huu ili tuweze kuutumia sote kwa pamoja mara baada ya matengenezo haya kukamilika”, alisema Malila.

Pia Malila aliwashukuru wadau mbalimbali wa Mbinga kwa kuunga mkono kwa njia ya kuwachangia fedha juu ya matengenezo hayo ambapo fedha hizo zimeweza pia kutumika kwa ajili ya kununua mafuta ya kuweka kwenye mitambo inayotumika kujenga uwanja huo na kulipia gharama nyingine.

Alisema kuwa Mbinga Veteran FC ina jumla ya wachezaji 30 ambao wanatoka katika sekta mbalimbali za serikali na binafsi ambapo anawaomba wadau hao waendelee kujitokeza kwa wingi kuunga mkono jitihada hizo ili matengenezo ya uwanja huo yaweze kukamilika kwa wakati na viwango bora vya kisasa.
 





No comments: