Saturday, March 25, 2017

SISTA KANISA KATOLIKI MBINGA AFIKISHWA MAHAKAMANI AKIDAIWA KUIBA MAMILIONI YA FEDHA ZA KANISA

Na Kassian Nyandindi,    
Mbinga.

KANISA Katoliki Jimbo la Mbinga wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limemfikisha Mahakamani Sista mmoja wa kanisa hilo ambaye anafahamika kwa jina la Emmanuela Nindi (40) kwa tuhuma ya kuliibia kanisa shilingi milioni 28.8 ambazo ni mali ya jimbo hilo.

Sista huyo ambaye alikuwa ni Mhasibu wa jimbo hilo, amefikishwa katika Mahakama ya wilaya hiyo kwa lengo la kumtaka ajibu shtaka hilo linalomkabili mbele yake.

Ilidaiwa na Mwendesha mashtaka wa Polisi Inspekta, Seif Kilugwe mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Mbinga, Magdalena Ntandu kwamba mshtakiwa huyo anadaiwa kufanya kosa hilo katika kipindi cha mwaka jana.


Inspekta Kilugwe alidai kuwa baada ya kutenda kosa hilo Sista Emmanuela alikimbia na kutokomea kusikojulikana, ndipo uongozi wa jimbo ulipofanya jitihada ya kumtafuta na baadaye uliweza kumpata na hatimaye kumfungulia mashtaka hayo.

Pia aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa Sista huyo alikuwa akiiba fedha hizo kidogo kidogo kwa nyakati tofauti hadi zilipofikia kiasi hicho, ambazo zilikuwa zinatokana na miradi ya jimbo pamoja na michango mbalimbali ya waumini wa kanisa hilo katoliki.


Hata hivyo mshtakiwa alipoulizwa mahakamani hapo juu ya kosa hilo analodaiwa kulifanya, alikana mashtaka hayo na kwamba alirudishwa mahabusu kutokana na kukosa wadhamini wawili wenye sifa ya kuweza kumdhamini ambapo shauri hilo litatajwa tena Machi 28 mwaka huu.

No comments: