Tuesday, March 28, 2017

SONGEA WAMUOMBA WAKALA WA DANGOTE KUANDAA MASHINDANO YA BONANZA MARA KWA MARA

Na Julius Konala,      
Songea.

BAADHI ya wananchi wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameuomba uongozi wa Chuo kikuu cha AJUCO Songea kupitia ufadhili wa Wakala wa usambazaji wa Saruji ya Dangote mkoani hapa, kuandaa mashindano ya bonanza mara kwa mara yatakayolenga kutafuta vijana wenye vipaji maalum ambao wataweza kushiriki katika mashindano mbalimbali yanayofanyika hapa nchini.

Wananchi hao walisema hayo mwishoni mwa wiki wakati walipokuwa wakizungumza kwa nyakati tofauti mjini Songea mara baada ya kuvutiwa na bonanza la michezo lijulikanalo kwa jina la, AJUCO Bonanza 2017 ambalo liliandaliwa na uongozi wa chuo hicho kupitia ufadhili wa Wakala wa usambazaji wa Saruji ya Dangote mkoani humo lililofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Majimaji mjini hapa huku washindi wa kwanza wakijinyakulia zawadi mbalimbali.

Bonanza hilo lilitanguliwa na michezo mbalimbali ikwemo kupanda milima ya Matogoro, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, mpira wa pete, mpira wa miguu pamoja na shindano la kumtafuta Miss and Mr. AJUCO 2017.


Kwa upande wa mchezo wa mpira wa miguu kulitanguliwa na mpambano kati ya timu ya AJUCO staff na AJUCO veteran ambapo mpaka mpira unakwisha AJUCO staff walikuwa wanaongoza kwa goli 1 lililofungwa na mwalimu Raymund Ndomba wakati AJUCO veteran wakigonga mwamba bila ya kuambulia goli.

Aidha bonanza hilo lilihitimishwa uwanjani hapo kwa mchezo wa mpira wa miguu katika shindano la fainali, kumtafuta mshindi wa kwanza mchezo ambao ulikuwa kati ya wanachuo wa mwaka wa kwanza na mwaka wa pili ambapo mpaka mpira unakwisha wanachuo mwaka wa kwanza walikuwa wanaongoza kwa magoli 2-1 na kutangazwa kuwa mshindi na kujinyakulia zawadi ya mbuzi mmoja na kombe.

Akizungumza katika bonanza hilo la michezo Ofisa masoko wa Wakala wa usambazaji wa Saruji ya Dangote mkoani Ruvuma mhandisi, Komba alisema kuwa lengo kubwa la kufanya bonaza hilo la michezo ni kuibua vijana wenye vipaji, kuinua kiwango cha michezo mkoani humo.


Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Dkt. Lognus Lutagwelela wakati alipokuwa akifunga mashindano hayo alimpongeza mfadhili huyo na waandaaji wa mashindano hayo akieleza kwamba mashindano yamekuwa yakijenga mahusiano, hukuza vipaji, hujenga afya pamoja na kuweka hamasa kwa wananchi kushiriki katika michezo.

No comments: