Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye akizungumza na waandishi wa habari (hawapo katika Picha) alipofanya ziara katika Chombo cha Habari cha Clouds Media Group leo Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye Katikati, akimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini (MOAT) Reginald Mengi (kulia) alipofanya ziara katika chombo cha Habari leo Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt. Hassan Abbas.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye (kulia) akijadiliana jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Joseph Kusaga (wa pili kushoto) alipowasili katika ofisi hizo leo Jijini Dar es Salaam, wengine ni Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo Dkt. Hassan Abbas (Pembeni ya Waziri) na wa kwanza kushoto ni Afisa Mahusiano wa Clouds Simon Simalenga.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye (katikati) akielezwa jambo na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Nchini (MOAT) Reginald Mengi (kulia) alipotembelea Ofisi hizo leo Jijini Dar es Salaam, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Joseph Kusaga.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye (kushoto) akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii Peter Serukamba (MB).
Wajumbe wa Kamati ya Maendeleo ya jamii wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati hiyo (hayupo katika picha) Peter Serukamba (MB) walipotembelea Kituo cha Habari cha Clouds leo Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu,
WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses
Nnauye ameunda Kamati ya watu watano itakayoongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya
Habari Maelezo Dkt. Hassan Abbas kuchunguza tukio la uvamizi lililofanywa na
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda katika chombo cha habari cha Clouds
Media.
Akiongea katika ziara aliyoifanya leo Jijini Dar
es Salaam katika chombo hicho Nape alisema kuwa Kamati hiyo itafanya kazi
ndani ya masaa 24 kuanzia sasa huku akiwataja wajumbe wengine kuwa ni
Frank Balile, Johanes Neng’ida, Jessy Kwayu na Mabel Mabisa kutoka Mamlaka ya
Mawasiliano Serikalini (TCRA).
“Kamati hii ipo kwa ajili ya kupata maelezo ya kutosha kutoka
kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ili tuwe na taarifa
iliyokamilika na kujua hatua itakayofuata”, alisema Nape.
Aidha Waziri Nape alieleza kuwa kitendo cha uvamizi
kilichofanywa na Mkuu wa Mkoa huyo kipo kinyume na Sheria ya Huduma ya Vyombo
vya Habari ya mwaka 2016 kwa kuwa sheria hiyo ipo kwa ajili ya kulinda
wanatasnia hao.
Aliongeza na kufafanua kuwa Serikali imesikitishwa na kitendo
hicho na ndio maaana akaunda kamati ya uchunguzi itakayokuja na taarifa kamili
huku akiwataka wanatasnia ya habari na wananchi kuwa watulivu na kusubiri
majibu ya uchunguzi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Habari ya Clouds,
Joseph Kusaga amemshukuru Waziri Nape kwa kuonyesha ushirikiano na kuwa pamoja
katika jambo hilo huku akifurahishwa na namna Serikali inavyowajali wadau wa
Habari.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari
Tanzania (MOAT) Reginald Mengi amempongeza Waziri huyo kwa hatua ya kuunda
kamati ya uchunguzi kwakuaanaamini itatoa matokeo chanya yatakayolinda heshima
ya Tasnia ya Habari nchini.
“Uamuzi wa kuunda kamati hii ni jambo la hekima na busara
linaloendana na misingi ya taaluma ya habari nasi tutakuwa radhi kuunga mkono
hatua zitachukuliwa katika kulinda uhuru wa habari nchini”, alisema
Mengi.
Tukio la kuvamiwa kwa kituo cha Clouds Media Group na Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam Paul Mkonda limetokea usiku wa Machi 17
mwaka huu.
No comments:
Post a Comment