Sunday, March 5, 2017

MBUNGE ATAKA KUREJESHWA KICHWA CHA NDUNA SONGEA MBANO

Waziri wa maliasili na utalii Profesa, Jumanne Magembe akiangalia juzi picha mbalimbali za marehemu mzee Rashid Kawawa (Simba wa vita) mara baada ya kuzindua rasmi makumbusho ya Kawawa eneo la Bombambili kata ya Bombambili katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.
Na Waandishi wetu,  
Songea.

MBUNGE wa viti maalum wanawake kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, Jaqcline Msongozi ameiomba serikali kupitia Waziri wa maliasili na utalii Profesa Jumanne Maghembe kuhakikisha kwamba inafanya juhudi za kuiomba serikali ya nchi ya Ujerumani kurejesha kichwa cha Nduna Songea Mbano.

Nduna Songea Mbano alikuwa Chifu wa kabila la Wangoni mkoani hapa ambaye  alifariki katika vita vya Majimaji mwaka 1905  pamoja na  Mashujaa wengine 66 na kwamba lengo la kukiomba kichwa hicho, ili kiweze kuoneshwa kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya vita hivyo kila mwaka hatua ambayo itasaidia hata vizazi vya sasa na vijavyo kuwa na uelewa juu ya tukio hilo.

Msongozi alitoa ombi hilo hivi karibuni mbele ya Waziri huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 110 ya Mashujaa wa vita hivyo yaliyofanyika katika eneo la Mahenge Manispaa ya Songea ambako wamezikwa Mashujaa hao.

Alisema kuwa wananchi na wazee wa mkoa wa Ruvuma, kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba kurejeshwa kwa kichwa cha Nduna Songea Mbano ili kiweze kuoneshwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo na kuwa kivutio halisi kwa Watalii kutoka maeneo mbalimbali, kwa madai kwamba hakuna sababu ya kichwa chake kuendelea kukaa Ujerumani wakati yeye ni Mtanzania.


Akizungumza na wananchi katika maadhimisho hayo Waziri wa maliasili na utalii Profesa Jumanne Maghembe amekubali ombi hilo na kufikisha kilio cha Mbunge huyo na wananchi wa mkoa wa Ruvuma, kwa Balozi wa Ujeruman nchini Tanzania Egon Kochanke ambapo ameonyesha kukubaliana na ombi hilo.

Maghembe aliwataka pia wananchi wa mkoa huo kutumia kumbukumbu ya Mashujaa wa vita vya Majimaji katika kuilinda na kuipigania amani ya Tanzania kwa nguvu zao zote kwa madai kwamba hakuna Taifa la nje litakaloweza kulinda amani hii tuliyonayo sasa.

Kadhalika Waziri huyo amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma kutumia fursa ya fukwe za ziwa Nyasa, katika kuwekeza hoteli mbalimbali kwa lengo la kuinua pato la mkoa na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na kwamba aliahidi kuboreshwa kwa vivutio hivyo ikiwemo ziwa hilo ambalo lina samaki wengi wa mapambo ambao hawapatikani popote pale duniani.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa wa vita vya Majimaji ambavyo vilipiganwa mnamo mwaka 1905 hadi 1907 yamesaidia kutoa fursa ya kukuza uchumi na kuvutia wawekezaji mkoani hapa.


Dkt. Mahenge alisema kuwa serikali ya mkoa huo itahakikisha kwamba inashirikiana na Wizara husika, ili kuyafanya makumbusho  hayo na yale ya Mzee Kawawa kuwa yenye hadhi ya kimataifa  na yatakayoweza kusaidia kukuza uchumi wa mkoa na nchi kwa jumla.

No comments: