Na Julius Konala,
Songea.
KATIKA kuadhimisha siku ya Wanawake duniani, Chama Cha Walimu
(CWT) kitengo cha wanawake Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kimetoa msaada wa
vitu mbalimbali kwa watoto wenye ulemavu ambao wana matatizo ya kusikia (Viziwi)
katika shule ya msingi maalum ya Mtakatifu Vincent Ruhuwiko iliyopo mjini hapa.
Msaada huo ulitolewa jana shuleni hapo na Mwenyekiti wa CWT
kitengo cha wanawake Manispaa ya Songea, Zabiuna Nchimbi ambapo alidai kuwa
wameamua kufanya hivyo baada ya kuguswa na tatizo hilo linalowakabili watoto
hao wenye ulemavu wa kusikia.
Nchimbi alitaja msaada uliotolewa kwa ajili ya watoto
hao kuwa ni viatu, nguo, mafuta ya kupaka, chumvi pamoja na sabuni za kufulia
huku akidai kuwa kufanikiwa kwa zoezi hilo kumetokana na kuchangishana walimu
wenyewe.
Awali akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti
huyo alisema kuwa walimu hao wanatambua changamoto mbalimbali wanazokumbana
nazo watoto hao wenye ulemavu wa kusikia, ndio maana wakaamua kuchangishana vitu
hivyo kwa lengo la kusaidia watoto hao ambapo ametoa rai kwa taasisi mbalimbali
kuona umuhimu wa kutembelea shuleni hapo kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mtakatifu
Vincent Ruhuwiko Sista Anna Mgaya, amekishukuru Chama hicho cha walimu kitengo
cha wanawake Manispaa ya Songea kwa msaada wao kwa madai kuwa imedhihirisha ni
jinsi gani wanavyowajali na kuwathamini watoto wenye ulemavu.
Mgaya alisema kuwa watoto hao wenye ulemavu wa kusikia
wanatakiwa kuthaminiwa na kwamba katika shule hiyo wapo watoto pia wenye vipaji
mbalimbali ambapo baadhi yao wamefanikiwa kufika mpaka elimu ya juu na vyuo vya
ufundi.
Hata hivyo Mwalimu mkuu huyo aliongeza kwa kusema kuwa
changamoto kubwa wanayokumbana nayo watoto hao ni baadhi ya madaktari na
watumishi mbalimbali, kushindwa kuwasiliana nao kwa alama pindi wanapougua na
kufuatilia huduma nyingine maofisini hivyo ametoa wito kwa jamii kujifunza
lugha za alama kwa lengo la kuwarahisishia kupata huduma kwa urahisi watoto
hao.
No comments:
Post a Comment