Wednesday, March 15, 2017

BREAKING NEWS: OFISA USHIRIKA HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA ABURUTWA MAHAKAMANI AKIDAIWA PEMBEJEO ZA WAKULIMA

Na Kassian Nyandindi,      
Mbinga.

KAIMU Ofisa ushirika wa Halmashauri wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, Kanisius Komba (36) leo amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya mwanzo Mbinga mjini wilayani humo, kwa tuhuma ya madai ya pembejeo za kilimo zenye thamani ya shilingi milioni 3,000,000.

Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Beatrice Mbafu alidai Mahakamani hapo kuwa mshtakiwa Komba alitenda kosa hilo katika kipindi cha mwezi Januari mwaka huu baada ya kushindwa kuwafikishia mifuko 100 ya mbolea aina ya UREA na SA wakulima wa vikundi vya VICOBA vilivyopo wilayani humo.

Ilidaiwa kuwa Ofisa ushirika huyo aliwaambia wakulima hao waingize fedha hizo kwenye akaunti namba 70810002597 benki ya NMB kwenda kwa Kampuni ya IWAWA Agrovet and General Supply iliyopo Jijini Dar es Salaam, ili waweze kupatiwa pembejeo hizo lakini mpaka sasa hawakuweza kupewa mbejeo zenye thamani ya fedha hizo.


Hakimu Mbafu aliieleza mahakama kuwa kutokana na madai hayo kufikishwa katika mahakama hiyo na mdaiwa kutokuwepo wakati shauri hilo linasomwa mahakamani hapo, wadai hao wanapaswa kumfikishia taarifa ili aweze kuhudhuria siku nyingine ambayo mahakama itapanga kwa ajili ya kusikilizwa.

Kadhalika baada ya hakimu huyo kutoa ufafanuzi huo msimamizi wa vikundi hivyo vya VICOBA wilayani Mbinga, Joyce Akitanda alisimama mahakamani hapo na kumweleza hakimu kwamba mdaiwa Komba alionekana akiranda randa nje katika maeneo ya mahakama hiyo ya mwanzo Mbinga mjini, lakini wanashangaa kutomuona akihudhuria wakati shauri hilo linatajwa mahakamani hapo.

Baada ya msimamizi wa vikundi hivyo kueleza hivyo, ndipo hakimu Mbafu alitoa ufafanuzi akidai kwamba kuna taratibu ambazo hazijakamilika na kuwekwa sawa ndiyo maana mdaiwa hawajaweza kumuona akihudhuria katika mahakama hiyo ya mwanzo, hivyo wanapaswa kuwa na subira na kumpatia taarifa mdaiwa huyo ili aweze kuhudhuria siku nyingine ambayo shauri hilo litatajwa tena.

Hata hivyo kesi hiyo imepangwa Machi 20 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa tena na kwamba mshtakiwa anapaswa kuhudhuria siku hiyo bila kukosa kabla hajachukuliwa hatua kali za kisheria.

No comments: