Na Mwandishi wetu,
Mtwara.
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema
kwamba mikutano ya kila baada ya miezi mitatu na kampuni zinazojihusisha na
utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia hapa nchini, itakuwa ikifanyika
maeneo mbalimbali nchini hususan kwenye rasilimali husika.
Waziri Muhongo aliyasema hayo hivi karibuni mkoani Mtwara
wakati wa mkutano wake na wawakilishi wa kampuni hizo, uliofanyika kwenye Kituo
cha kuchakata gesi asilia cha Madimba mkoani humo.
Alisema kuwa mikutano hiyo mara zote ilikuwa ikifanyika Jijini
Dar es Salaam hivyo ili kuweza kuleta tija zaidi ni vyema ikafanyikia kwenye
maeneo yenye gesi asilia na baadaye siku za usoni itafanyika kwenye maeneo
yatakayogundulika kuwa na mafuta.
Kadhalika aliongeza kuwa kila baada ya miezi mitatu
kumekuwepo na utaratibu wa kukutana kwa ajili ya kutathimini maendeleo ya miradi
husika na kila kampuni itakuwa ikiwasilisha ratiba yake ya kazi ambayo itajadiliwa.
“Hii mikutano kila kampuni itakuwa ikitupatia ratiba yake ya
kazi, tunaijadili na kushauriana endapo kama wana matatizo tunatafuta
suluhisho,” alisema Waziri Muhongo.
Waziri Muhongo alisema shughuli za utafutaji, uvunaji na
uendelezaji wa gesi asilia na mafuta zinaendelea vizuri huku majadiliano
mbalimbali yakiendelea kuhusiana na utekelezaji wa miradi hiyo.
No comments:
Post a Comment