Na Kassian Nyandindi,
Songea.
KATIKA kuhakikisha kwamba serikali inaendelea kuviwezesha
vikundi vya vijana na wanawake hapa nchini, mkoa wa Ruvuma kupitia halmashauri
zake nane zilizopo mkoani humo imetenga shilingi milioni 335.6 kwa mwaka wa
fedha wa 2016/2017 ili vikundi hivyo viweze kujiinua kiuchumi na kusonga mbele
kimaendeleo.
Katika fedha hizo tayari mikopo ya shilingi milioni 90.5
imetolewa kwa vikundi vya vijana 2,619 vyenye wanachama 1,292 ambao wamenufaika
na mikopo ya fedha za mfuko wa maendeleo ya vijana pamoja na fedha za mapato ya
ndani ya halmashauri husika ndani ya mkoa huo.
Mkoa wa Ruvuma unakadiriwa kuwa na vijana 672,540 sawa na
asilimia 48 ya wakazi wa mkoa huo wapatao milioni 1,376,891 kulingana na sensa
ya watu na makazi ya mwaka 2012 na wastani wa ongezeko la watu kila mwaka.
Hayo yalisemwa na Kaimu Katibu tawala wa mkoa huo, Bwai
Biseko alipokuwa akitoa taarifa ya shughuli za maendeleo ya vijana mkoani hapa
kwenye mafunzo elekezi ambayo yalijumuisha vijana hao kutoka mikoa mitatu ya
Ruvuma, Lindi na Mtwara yaliyofanyika katika Manispaa ya Songea mjini hapa.
Biseko alisema kuwa vijana wengi wamekuwa wakijishughulisha
na shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo cha kahawa, korosho, mahindi,
mpunga upandaji miti ya mbao, kilimo cha soya, mbaazi, uvuvi, bustani za mboga
mboga pamoja na biashara za kuuza bidhaa ndogo ndogo kwa lengo la kukuza maisha
yao yaweze kusonga mbele kupitia mikopo hiyo wanayoipata kwenye vikundi vyao.
Aidha alieleza kuwa mkoa huo unaendelea kutekeleza majukumu
yake ya kila siku ikiwa ni pamoja na kuhamasisha vijana hao, kujiunga na
vikundi vya uzalishaji mali ambavyo kupitia halmashauri za wilaya vimetambuliwa
na baadhi yake huendelea kupewa mikopo.
Akizungumzia juu ya utengaji wa maeneo ya shughuli za vijana,
mikopo ya mfuko wa maendeleo ya vijana pamoja na asilimia tano ya mapato ya
ndani ya halmashauri, Biseko aliongeza kuwa halmashauri zote za mkoa huo wilaya
ya Madaba, Mbinga vijijini, Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Songea vijijini, Manispaa
ya Songea na halmashauri ya mji wa Mbinga tayari zimetenga fedha kwa ajili ya
kutoa mikopo kwa vijana na akina mama.
Kadhalika alibainisha kuwa halmashauri ya Madaba imetenga
shilingi milioni 12.5 kwa vikundi saba kati ya vikundi 21, Manispaa ya Songea
imetenga shilingi milioni 26.4 na vikundi 10 vimepata mkopo wa shilingi milioni
10 kwa ajili ya biashara ndogo ndogo, mama lishe na boda boda na tayari
imetenga ekari tisa na kutolewa kwa wafanyabiashara wadogo katika kata ya Msamala,
Majengo na Ruhuwiko.
Alitaja halmashauri nyingine kuwa ni Songea vijijini
iliyotenga na kutoa shilingi milioni 10 kwa vikundi vitano kati ya 255 vya
vijana vilivyopo wilayani humo kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na
biashara ndogo ndogo.
Vilevile halmashauri ya wilaya ya Nyasa katika bajeti yake
imetenga shilingi milioni 25.7 ambazo bado hazijapelekwa kwa wahusika na kwamba
tayari imetenga pia eneo kwa ajili ya shughuli za kilimo cha zao la Cocoa, umwagiliaji
mpunga na kilimo cha zao la kahawa.
Biseko alisema kuwa halmashauri ya mji wa Mbinga imetenga
shilingi milioni 4 na tayari imekwisha toa kwa kikundi cha vijana kimoja
kilichopo mjini hapa, Namtumbo imetenga shilingi milioni 57 na fedha
iliyotolewa katika fedha hizo tayari shilingi milioni 12 zimekwenda kwa vikundi
21 sambamba na kutenga eneo la ekari 331.39 katika kata ya Rwinga na Namtumbo
kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Hata hivyo alieleza kuwa changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni
upungufu wa maofisa vijana kwani mkoa una upungufu wa maofisa sita kati ya
wanane wanaohitajika kwenye halmashauri, elimu ya ujasiriamali bado
haijawafikia vijana wengi, ukosefu wa soko la uhakika hasa kwa mazao ya chakula
na biashara na ukosefu wa mitaji ya kuanzisha na kuendesha miradi ya
vijana.
No comments:
Post a Comment