Tuesday, March 28, 2017

MPITIMBI SONGEA WAJITOKEZA KUTAKA KUPIMIWA MASHAMBA YAO

Na Julius Konala,    
Songea.

ZAIDI ya wananchi 40 wakiwemo wakulima wadogo wadogo katika kijiji cha Mpitimbi A wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, wamejitokeza na kutaka kupimiwa maeneo yao ya mashamba kwa lengo la kupata Hati ya hakimiliki ya kimila baada ya kupewa elimu juu ya matumizi bora ya ardhi, ambayo ilitolewa na shirika lisilokuwa la serikali MVIWATA lililopo mkoani hapa.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Michael Ponera alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu kijijini humo, akielezea juu ya mwitikio wa wananchi wake namna walivyojitokeza na kuupokea mpango huo mara baada ya kupata elimu hiyo.

Ponera alisema kuwa wananchi hao tangu wapate elimu hiyo juu ya kuweza kutambua masuala ya sheria na umuhimu wa upimaji ardhi sasa wamekuwa wakijitokeza na kujiorodhesha majina yao katika ofisi ya kijiji hicho, wakitaka wapimiwe maeneo yao na kwamba watakapofikia 200 zoezi hilo la upimaji litaanza kwa kuwashirikisha wataalamu wa ardhi kutoka halmashauri ya wilaya ya Songea iliyopo mkoani humo kwa ajili ya kuweza kuwapimia mashamba yao.


Alieleza kuwa kufanikiwa kwa mpango huo utakuwa ni mkombozi mkubwa na muarobaini wa kupunguza migogoro ya ardhi na mipaka kati ya mtu na mtu, kijiji na kijiji pamoja na kuondoa kabisa suala la uvamizi holela wa maeneo ya ardhi.

Naye mmoja wa wananchi wa kijiji hicho cha Mpitimbi, Longnus Mtewele amelishukuru shirika hilo kwa kutoa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo huku akifafanua kuwa kabla yake hawakuwa na uelewa wowote juu ya umuhimu wa masuala ya upimaji ardhi na kwamba baada ya kupata elimu hiyo wameweza kujua sheria na thamani ya ardhi ndio maana wamehamasika ili waweze kupimiwa mashamba yao.

Alisema kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo hivi sasa wanashindwa kumudu gharama za upimaji wa ardhi ambapo wameiomba serikali kuwasaidia kulipia gharama hizo, ili waweze kupata Hati ya hakimiliki ya kimila zitakazoweza kuwasaidia kupata mikopo kutoka kwenye taasisi mbalimbali za kifedha na kuwawezesha kufanyia shughuli mbalimbali za kimaendeleo.


Kwa upande wake Ofisa habari wa shirika hilo Denis Mpagaze alisema kuwa toka mpango huo uanze kutekelezwa kwa kipindi cha miezi sita iliyopita wameweza kuwafikia watu 200 kutoka vijiji vya Magagura, Mpandangindo, Mpitimbi na Mbinga Mhalule wilayani Songea.

No comments: