Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Binilith Mahenge. |
Na Muhidin Amri,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amewataka viongozi
kuanzia ngazi ya vitongoji hadi wilaya, wahakikishe kwamba wanadhibiti kikamilifu
matumizi ya pombe zilizofungashwa kwenye mifuko maarufu kama Kiroba ili zisiweze
kuonekana mitaani zikiendelea kutumika, ikiwa ni lengo la kuokoa maisha ya Watanzania
wengi hasa vijana walioathirika na matumizi ya pombe hizo.
Dkt. Mahenge alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi
wa habari mjini hapa, ambapo alieleza kuwa matumzi ya viroba yamekuwa yakichochea
pia ongezeko la matukio ya uhalifu na ajali barabarani, hasa kwa zile zinazotokana na waendesha
pikipiki maarufu kwa jina la bodaboda na kusababisha watu wengi kuumia, kupoteza
viungo vyao vya mwili kuwa walemavu huku wengine wakipoteza maisha yao.
Alisema kuwa hata baadhi ya maeneo wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari wamekuwa wakiacha kuzingatia masomo yao darasani badala
yake wamekuwa vinara wakubwa wa kunywa pombe hizo, jambo ambalo linahatarisha
hapo baadaye kuwa na taifa la watu goigoi ambao watashindwa kumudu kufanya kazi
za kujiletea maendeleo.
Mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, Dkt. Mahenge alifafanua kuwa
matumzi ya kiroba yamekuwa yakisababisha athari mbalimbali hasa kwa vijana
ambao hununua pombe hiyo kutokana na urahisi wa bei yake, hivyo ameliagiza
Jeshi la Polisi na vyombo vyote vya ulinzi na usalama mkoani humo kufanya doria
mara kwa mara hasa maeneo ya mipakani na sehemu za starehe ili kuweza kudhibiti
kabisa matumzi ya pombe hiyo na kwa yule atakayekamatwa akiuza achukuliwe hatua
za kisheria ikiwemo kufikishwa Mahakamani.
No comments:
Post a Comment