Kamishna
msaidizi wa Polisi ACP Advera Bulimba.
|
Na Frank Geofray - Jeshi la Polisi.
MAOFISA Wakuu wa Polisi wanatarajia kukutana mkoani
Dodoma kuanzia Jumatatu Machi 27 hadi 29 mwaka huu, katika kikao kazi cha siku
tatu kujadili na kupanga mikakati mbalimbali ya kukabiliana na uhalifu hapa
nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake, Msemaji wa
Jeshi la Polisi Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Advera Bulimba alisema
kikao hicho kitawakutanisha maofisa wakuu wa makao makuu ya Polisi, makamanda
wa Polisi wa mikoa na Makamanda wa vikosi vya bara na Zanzibar ili kujadili
mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utendaji kazi kipindi cha mwaka
uliopita na kuweka mikakati mipya ya kupambana na uhalifu kwa mwaka huu 2017.
Aidha, Bulimba alisema kwamba mbali na utaratibu wa
mawasiliano ya kila siku katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao, Jeshi
la Polisi pia lina utaratibu wa kukutana kila mwaka kwa pamoja ili
kubadilishana uzoefu wa kukabiliana na wahalifu kwa lengo la kuhakikisha kuwa
usalama wa raia na mali zao unaendelea kuimarika hapa nchini.
“Katika kikao hicho Inspekta Jenerali wa Polisi IGP Ernest
Mangu atatoa maelekezo ya kiutendaji ambayo lengo lake ni kuhakikisha pia kila
ofisa, mkaguzi na askari wake anawajibika kwa nafasi yake katika kuhakikisha
uhalifu unapungua hapa nchini”, alisema Bulimba.
Bulimba alisema kikao kazi hicho kinatarajiwa kufunguliwa na
Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba ambapo kauli mbiu katika
kikao hicho ni “Zingatia maadili tunapopambana na uhalifu ili kuimarisha
usalama kwa maendeleo ya Taifa”.
No comments:
Post a Comment