Na Mwandishi wetu,
Songea.
KWA nyakati tofauti Wakazi wa Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma, wamelaani kitendo cha baadhi ya Wafanyabiashara wa Soko kuu Songea
kukosa uzalendo na kushindwa kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano,
katika kufanikisha suala la ukusanyaji wa mapato yake.
Aidha walisema kuwa badala yake wafanyabiashara hao wamekuwa
wakihusika moja kwa moja kushinikiza watu wengine kukataa ongezeko la kodi
mpya ya vibanda katika Soko hilo, kwa ajili ya maslahi yao binafsi huku
wapangaji wengine wakijinufaisha kutokana na pango wanalopokea jambo ambalo linaisababishia
serikali hasara kubwa.
Walisema kuwa kitendo cha wapangaji hao kugomea
ongezeko hilo jipya la pango katika vibanda hivyo linaonesha
ni jinsi gani baadhi ya watu wanavyotaka kujinufaisha kupitia migongo ya watu wengine,
kwani haiwezekani Manispaa ya Songea ikapata fedha
kidogo na watu walioingia mikataba kwa kuwatumia madalali
wakiendelea kunufaika kuwapangisha watu wengine kwa fedha nyingi.
Hivi karibuni wafanyabiashara wa Soko kuu la Manispaa hiyo walijikuta
katika mgogoro mkubwa na uongozi husika wa Manispaa baada ya kugomea bei mpya
ya pango inayotakiwa kulipwa kwa Manispaa badala ya madalali ambao wamekuwa
wakijinufaisha kupitia mgongo wa nyuma.
Wakizunguza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti mjini hapa walisema
kuwa kitendo kilichofanywa na wafanyabiashara hao kuchelewa kujaza maombi kwa
ajili ya kuendelea na shughuli zao za kila siku katika soko hilo hakikuwa cha
kiungwana kwa sababu wananchi wanakosa huduma na mahitaji
muhimu ya kila siku.
Walisema kuwa haiwezekani Manispaa ambayo ndiyo mmiliki
halali wa vibanda hivyo hupata pango la shilingi 108,000 kwa mwezi wakati
wapangaji hupangisha watu wengine kwa fedha nyingi kati ya shilingi 350,000
hadi 450,000 tena bila kuilipia kodi serikalini.
Kassiana Ngonyani (42) mkazi wa Mateka alisema kuwa hatua ya
Manispaa kufunga vibanda vya wafanyabiashara katika soko hilo ilikuwa ni jambo
jema kwani kwa muda mrefu ilijikuta ikipata hasara kubwa huku baadhi ya watu
wakinufaika licha ya kutoingia gharama yoyote.
Ngonyani alieleza kuwa kitendo baadhi ya wapangaji waliokuwa
na mikataba na Manispaa kuwapangisha watu wengine hakikuwa sahihi kwani utaratibu
unaeleza kwamba mtu mwenye mamlaka halali ya kupangisha ni Manispaa na sio mtu
binafsi.
Christian Kanjolonga yeye mbali na kuupongeza
uongozi wa Manispaa hiyo kwa uamuzi wake wa kufunga vibanda hadi pale wafanyabiashara
watakapojaza mikataba mipya alisema kuwa ni uamuzi sahihi na amewataka
wananchi wengine kutambua kuwa, serikali ya awamu ya tano imekuja na
mikakati yake hasa katika ukusanyaji thabiti wa kodi au mapato yake.
Aliongeza kuwa tabia ya kufumbiana macho na
kuoneana aibu na wakati mwingine kubebana ndiyo kunakosababisha Manispaa
ya Songea kuwa kati ya halmashauri maskini hapa nchini, licha ya kuwa na vyanzo
vingi vya mapato ambavyo kama vingesimamiwa vizuri vingeweza kusaidia kuharakisha
maendeleo ya kukuza uchumi pamoja na kuboresha huduma za kijamii.
“Lazima wananchi wenzangu wanapaswa kuelewa kwamba, serikali
ya awamu ya tano ni tofauti kabisa na serikali zilizotangulia ni vyema sasa kujifunza
kulipa kodi na maduhuli mengine ya serikali kwa wakati”, alisema Kanjolonga.
Pamoja na mambo mengine hivi sasa wafanyabiashara na
wapangaji wa vibanda hivyo vya Soko kuu la Songea, wanaendelea na shughuli zao
baada ya kuingia mikataba mipya ya upangaji na Manispaa ya Songea kutokana na kumaliza
tofauti zao zilizokuwepo hapo nyuma.
No comments:
Post a Comment