Wednesday, March 8, 2017

CCM RUVUMA WAITAKA SERIKALI KUSIMAMIA KIKAMILIFU UJENZI WA DARAJA MTO RUHUHU

Na Kassian Nyandindi,    
Nyasa.

KAMATI ya siasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Ruvuma, imeitaka serikali kupitia Wakala wake wa barabara (TANROADS) mkoani humo kusimamia kikamilifu ujenzi wa daraja la mto Ruhuhu, lililopo wilayani Nyasa mkoani hapa na kumuhimiza mkandarasi anayejenga daraja hilo akamilishe ujenzi wake kwa wakati na viwango vinavyokubalika.

Aidha kampuni ya ujenzi Lukolo Construction Limited ndiyo inayofanya kazi ya ujenzi wa daraja hilo, ambapo Wajumbe wa Kamati hiyo walitembelea juzi kuona maendeleo ya mradi huo, ambao upo katika kata ya Lituhi wilayani humo mpakani mwa mkoa wa Ruvuma na wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe.

Mjumbe mmoja ambaye ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho alisema kuwa serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kikamilifu kwa kuhakikisha kwamba, inaondoa kero zilizopo kwa wananchi wake wanaoishi katika maeneo hayo ndio maana inajenga daraja hilo hivyo mkandarasi huyo anapaswa kufanya jitihada kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya mkataba husika.

Napegwa Kiseko ambaye ni Mhandisi mshauri ujenzi wa daraja hilo aliiambia Kamati hiyo ya siasa ya Chama Cha Mapinduzi kwamba mradi huo ujenzi wake unafadhiliwa kwa asilimia mia moja na serikali ya Tanzania.

“Daraja hili linalojengwa hapa, lipo umbali wa kilometa 84 kutoka kijiji cha Kitai wilaya ya Mbinga ambako kuna barabara kuu ya kiwango cha lami, tutahakikisha tunasimamia na kushauri kwa umakini mkubwa ili liweze kukamilika kwa viwango vinavyokubalika na wananchi waweze kuanza kulitumia”, alisema Kiseko.


Alisema kwamba mradi huo hadi kukamilika kwake utachukua miezi 24 na kwamba utakapokamilika utatatua kwa kiasi kikubwa  kikwazo cha kutokuwa na mawasiliamo ya uhakika yaliyodumu kwa muda mrefu kati ya wananchi wa mkoa wa Ruvuma na Njombe na hatimaye kuweza kuchochea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Alifafanua kuwa mradi huo ulianza kutekelezwa Juni 17 mwaka jana chini ya usimamizi wa Ofisi ya Meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma na kwamba wakati mchakato wa kumpata mhandisi mshauri ulipokuwa unaendelea, Februari 6 mwaka huu kampuni ya Crown Tech-Consult Limited kutoka Jijini Dar es salaam ilisaini mkataba wa makubaliano ya usimamizi wa mradi huo.

Mhandisi Kiseko alieleza kuwa mkataba huo unahusisha usimamizi ujenzi wa msingi  wa daraja, kuta mbili za pembeni na nguzo mbili zitakazokuwa ndani ya mto na kwamba daraja hilo litakuwa na midomo mitatu yenye jumla ya urefu wa mita 98 na kazi nyingine ni ujenzi wa box kalavati moja lenye midomo miwili na visaidizi vya daraja hilo.

Awali Meneja wa TANROADS mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Allynanuswe Razaq  alipokuwa akitoa taarifa ya hali ya mtandao wa barabara mkoani humo alisema kuwa kwa mujibu wa ukaguzi uliofanyika mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana, unaonesha kwamba hali ya barabara kuu zenye kiwango cha lami kwa ujumla zina hali nzuri kutokana na kufanyiwa matengenezo ya mara kwa mara pale zinapoharibika.

Alisema kuwa mpango wa TANROADS Ruvuma ni kuendelea kukarabati barabara zote ambazo zina maeneo korofi kwa kuhakikisha maeneo hayo yanapitika kipindi chote cha masika au kiangazi.

Pamoja na mambo mengine, wakati wa Kampeni za uchaguzi Mkuu mwaka 2015, mgombea Urais kwa tiketi ya CCM ambaye ndiye Rais wa Tanzania, John Magufuli alisema anatambua adha wanayopata wananchi wa Lituhi na Lipingu vijiji vilivyotenganishwa na mto huo kutokana na kivuko kilichopo kushindwa kufanya kazi ipasavyo kutokana na maji kupungua.


Hivyo kufuatia kuwepo kwa adha hiyo, Rais Magufuli alisema baada ya kuingia madarakani ujenzi wa daraja hilo utakuwa miongoni mwa vipaumbele vyake kwa kuwa ipo kwenye ilani ya uchaguzi ni lazima itekelezwe na sasa hatimaye daraja hilo linajengwa na serikali hii ya awamu ya tano.

No comments: