Jackline Msongozi akizungumza juzi siku ya sherehe za maadhimisho ya wanawake duniani mjini Songea. |
Na Julius Konala,
Songea.
MBUNGE wa Viti maalum Wanawake mkoani Ruvuma, Jackline Msongozi
kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameipongeza serikali ya awamu ya
tano kupitia Wakala wake wa barabara Tanroads mkoani hapa, kwa kusimamia na kukamilisha
ujenzi wa barabara kiwango cha lami inayounganisha upande wa Mangaka mkoani
Mtwara hadi Namtumbo mkoani Ruvuma kwa madai kuwa baadhi ya wanawake wameanza
kunufaika na mradi huo kiuchumi kutokana na kuuza bidhaa mbalimbali.
Msongozi alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza
kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani ambapo kiwilaya yalifanyika
katika viwanja vya soko la Mjimwema lililopo mjini Songea.
Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumechochea kasi ya
maendeleo kwa akina mama wajasiriamali kujiinua kiuchumi kutokana na kuanzisha
biashara ndogo ndogo pembezoni mwa barabara hiyo pamoja na kusafirisha mazao
yao kwa urahisi.
Aidha amewataka wanawake hao kutumia fursa ya kukamilika kwa
miradi ya ujenzi wa barabara, kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali
ikwemo katika nyanja ya kilimo na ufugaji kwa lengo la kujipatia kipato badala
ya kuwa tegemezi.
Mbali na mambo mengine Mbunge huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi
kwenye maadhimisho hayo, amewapongeza pia wanawake hao kwa kuonesha moyo wa
ujasiri katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi za kisiasa mkoani humo.
Awali akisoma risala kwa niaba ya wanawake wenzake
mbele ya mgeni rasmi, Joyce Mwanja alisema kuwa kutokana na uhamasishaji wa
wanawake wengi kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali kumesaidia kuongeza
uelewa na ari ya utendaji kazi kiuchumi ambapo jumla ya vikundi 300
vya wanawake wazalishaji mali vimeundwa mjini hapa.
Mwanja alisema kuwa katika kipindi hicho chote shughuli
mbalimbali za uzalishaji mali zimefanyika ikiwemo usindikaji, kilimo, uanzishwaji
wa magenge ya kuuzia biashara, ufugaji, kilimo, ufumaji na uhifadhi wa
mazingira ambapo katika kipindi cha mwaka 2014/2015 hadi mwaka 2016/2017 jumla
ya vikundi 172 vya wanawake wajasiriamali vimepatiwa mikopo midogomidogo yenye
masharti nafuu yenye thamani ya shilingi milioni 87.1.
No comments:
Post a Comment