Na Muhidin Amri,
Songea.
WAKALA wa Barabara (TANROAD) mkoani Ruvuma amesema kwamba
kuanzia mwezi Januari mwaka 2013 hadi kufikia Januari mwaka huu, ametumia jumla
ya shilingi bilioni 2,011,195,000 ikiwa ni gharama ya ulinzi wa mitambo
iliyoachwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Progressive Higleig ya kutoka nchini India.
Imeelezwa kuwa gharama hizo zimetokana na kuwalipa askari
Polisi waliokuwa wakilinda mitambo ya kampuni hiyo katika maeneo mbalimbali ya
mradi kwa kipindi cha miaka minne, baada ya serikali kumfukuza mkandarasi huyo kutokana
na kushindwa kujenga barabara ya kutoka wilaya ya Namtumbo hadi Tunduru mkoani
hapa kwa kiwango cha lami.
Meneja wa TANROAD wa mkoa huo, Razack Alinanuswe alisema hayo
juzi alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake na kuongeza kuwa
serikali imeingiza shilingi bilioni 4,319,452,900 baada ya kuuza mitambo hiyo
kwa njia ya mnada kwa watu binafsi na taasisi mbalimbali.
Alisema kuwa baada ya serikali kumfukuza mkandarasi huyo
kutokana na kushindwa kwake kufanya kazi hiyo aliyopewa, ililazimika
kushikilia mitambo yake na Wakala huyo wa barabara mkoani hapa na kubeba jukumu
la kuilinda kwa muda wote kwa kutumia Jeshi la Polisi ambalo lilifanya kazi kwa
uadilifu mkubwa licha ya kuwepo kwa baadhi ya changamoto mbalimbali.
Pia Alinanuswe alifafanua kuwa serikali iliuza mitambo hiyo
kwa njia ya mnada kwa lengo la kuepuka ongezeko la gharama kubwa kama vile ulinzi,
pamoja na kuendelea kusimamia sheria ya hifadhi ya barabara ili kuhakikisha
kwamba watu hawajengi katika hifadhi ya barabara hiyo.
Vilevile alibainisha kuwa mkoa wa Ruvuma changamoto
kubwa inayokabiliana nayo katika kazi za ujenzi wa miradi ya barabara za lami
ni upungufu wa changarawe, udongo mzuri kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya
barabara hizo jambo ambalo wataalamu hulazimika kuchanganya kifusi na saruji au
chokaa ili kuongeza ubora.
Kwa mujibu wa Meneja huyo wa Wakala wa barabara mkoani
Ruvuma, alieleza kuwa tatizo lingine ni upungufu wa fedha kwani mkoa umekuwa
ukipokea fedha pungufu kuliko mahitaji husika, hasa kwa ajili ya matengenezo ya
madaraja na shughuli zingine za utawala.
Hata hivyo alisema kuwa mbali na matatizo hayo pia kwa muda
mrefu mkoa unakabiliwa na uwepo wa uwezo mdogo wa wakandarasi wa kazi za ujenzi
wa barabara za lami, pia wakandarasi hao kuchelewa kujipanga kwa vifaa vya
mitambo ya ujenzi na kokoto za matengenezo ya barabara hizo.
No comments:
Post a Comment