MKUU wa mkoa wa Ruvuma Dkt. Binilith Mahenge amelitaka Jeshi
la Polisi mkoani humo, kuhakikisha kwamba linasimama imara na kuongeza nguvu
hasa katika maeneo ya mipakani ili kuweza kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za
kisheria watu wanaoingiza madawa ya kulevya kupitia mipaka ya mkoa huo.
Aidha Dkt. Mahenge ameviagiza vyombo vyote vya ulinzi na
usalama mkoani hapa kuhakikisha vinashirikiana na Polisi kufanya msako mkali utakaoweza
kufanikisha kuwakamata baadhi ya watu wanaotumia, kuuza na kusafirisha madawa hayo
kutoka ndani na nje ya nchi.
Dkt. Mahenge alisema kuwa mapambano dhidi ya madawa ya
kulevya ni magumu, hivyo kila mwananchi lazima ashiriki kikamilifu bila kujali
wahusika wa biashara hiyo ni watu wa aina gani, cheo au mchango wao katika
jamii inayotuzunguka.
Alisema kuwa madhara ya madawa ya kulevya katika jamii yetu
ni makubwa mno ambapo baadhi ya familia zimepoteza vijana wao ambao ni nguvu
kazi na sio kwa familia hizo tu, bali hata kwa taifa letu jambo ambalo
limechangia kuendelea kuwa maskini.
Pia aliwataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma, wakiwemo waandishi
wa habari kutoa taarifa sahihi zitakazofanikisha kukamatwa kwa watu hao huku
akiongeza kuwa, madawa hayo ni janga kubwa katika nchi yetu na kwamba viongozi
waliopo katika ngazi ya vijiji, kata na wilaya nao wametakiwa kushiriki
kikamilifu katika kupambana na vita hiyo ambayo imeanzishwa na serikali hii ya
awamu ya tano.
Dkt. Mahenge amewaagiza wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa
Songea, ofisi za uhamiaji na bandari ya Mbamba bay wilayani Nyasa mkoani humo, kuongeza
juhudi na umakini mkubwa wa kufanya upelelezi na upekuzi wa watu wanaoingia
na kutoka katika maeneo hayo.
No comments:
Post a Comment