JESHI la Polisi limesema kwamba limeanza kufanyia kazi
maagizo waliyopatiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba,
kumsaka mtu aliyemtolea bastola aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye.
Hayo yalisemwa jana na Msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso
ambapo awali, alipotafutwa Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Ernest Mangu, lakini simu
yake ilipokelewa na msaidizi wake aliyemtaka mwandishi amtafute Msemaji wa
Jeshi la Polisi, Advera Senso ili atoe ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa agizo la
Waziri Nchemba.
Alipopigiwa simu, Senso alijibu kwa ufupi kuwa wameanza
kufanyia kazi agizo la Waziri Nchemba.
“Sisi tumepokea maelezo ya waziri na tayari tumeanza
kuyafanyia kazi, hilo ndilo ninaloweza kukwambia,” alisema.
Hali hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Polisi
aliyevalia kiraia kumtishia bastola, Nape ambaye pia ni Mbunge wa Mtama (CCM).
Waziri Nchemba alilaani kitendo hicho na kumuagiza Mkuu wa
Jeshi la Polisi kuchukua hatua “Mheshimiwa Nape sio jambazi, hana rekodi za
uhalifu. Kitendo cha kutolewa bastola si cha Kitanzania na si cha kiaskari na
sio cha Kimungu,” ameandika Mwigulu katika ukurasa wake wa facebook.
“Kama mtu ameweza kutoa bastola mbele ya kamera, nawaza
mbali, ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini. Nimemuagiza IGP achukue hatua.
“Nahusika na usalama wa raia wote wa Tanzania. Nimemwelekeza
IGP atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia
ya uaskari. Na kama ni askari, basi sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue
mkondo wake.”
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment