Na Julius Konala,
Songea.
MTANDAO wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) mkoani
Ruvuma, kupitia ufadhili wa shirika la Tanzania Foundation for Civil Society (FCS)
umeendesha mafunzo juu ya matumizi bora ya ardhi kwa wakulima wadogo wadogo wanaotoka
katika kata nne wilayani Songea mkoani humo.
Mafunzo hayo yalifanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa
chuo cha ushirika kilichopo katika Manispaa ya Songea ambayo yalifunguliwa na
Mwenyekiti wake Asumpta Ndauka, ambapo washiriki hao wametakiwa kuzingatia sheria
na taratibu husika za mafunzo hayo waliyopata kwani wao ndio waathirika wakubwa
wa migogoro ya ardhi vijijini.
Aidha mafunzo hayo yalishirikisha washiriki 200 wa kutoka
katika kata ya Magagura, Mpitimbi, Mpandangindo na Mbingamhalule wilayani humo
na kwamba Mwenyekiti huyo amewataka pia wanawake kuwa mstari wa mbele katika
kupigania haki zao juu ya umilikishwaji wa ardhi na kupata hati miliki kwa
madai kuwa wao wamekuwa wakikosa fursa hiyo kutokana na uwepo wa tatizo la
mfumo dume.
“Hivi sisi wanawake kwetu ni wapi, maana kwa upande wa wazazi
wetu tunakosa fursa ya kumiliki ardhi na kwa waume zetu hatuna nafasi ya
kumiliki ardhi jambo hili linatufanya tushindwe kuelewa nafasi yetu katika
suala la umiliki wa ardhi lipo wapi”, alihoji Ndauka.
Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Leonce Mutalemwa aliwataka
washiriki hao wa vikundi vya wakulima kutambua kuwa suala la umiliki wa ardhi
ni haki ya kila mmoja iwe mwanaume au mwanamke, huku akiwaasa
washiriki hao kuwa na hati ya pamoja kwa mali isiyogawanyika kwa madai kwamba
kufanya hivyo kutasaidia kuondoa migogoro katika familia na kumlinda mjane au
mgane.
Wanufaika hao wa vikundi vya wakulima kutoka katika kata hizo
wameweza kujifunza mada mbalimbali ikiwemo kujua sheria za ardhi Tanzania na
kutambua thamani ya ardhi.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki hao, Pascal Kilawi kutoka
kata ya Mpitimbi, Prisca Mhagama kutoka kata ya Magagura na Dionis Geo
walipokuwa wakihojiwa na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti walisema kuwa
mafunzo hayo yameweza kuwajengea uwezo wa ufahamu juu ya masuala ya ardhi, ambapo
miongoni mwao wameanza kupata mwanga katika kupata haki zao na kwamba
wanakumbana na changamoto ya kupata ushirikiano mdogo toka ofisi za vijiji na
wananchi wengi kushindwa kumudu gharama za upimaji na upatikanaji wa hati
miliki.
No comments:
Post a Comment