Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
IMEELEZWA kuwa vitendo vya kuendekeza ngoma za asili, mila na
desturi nyakati za mchana na usiku katika wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,
vimekuwa vikichangia na kuleta athari kubwa kwa watoto wa kike na kusababisha
watoto hao kukatisha masomo yao kutokana na kupata ujauzito.
Luckness Amlima. |
Aidha tatizo hilo imefafanuliwa kuwa linachangiwa na wazazi,
hivyo watoto wanashindwa kuzingatia masomo badala yake wamekuwa wakishiriki
kwenye ngoma hizo jambo ambalo limekuwa likirudisha nyuma maendeleo yao
kitaaluma pale wanapokuwa darasani.
Luckness Amlima ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo alisema hayo juzi
wakati alipokuwa akimweleza mwandishi wetu, juu ya mikakati ya kupambana na vitendo
vya mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili waweze kuendelea na
masomo yao.
Alisema kuwa mkakati mojawapo katika kukabiliana na tatizo
hilo ni kwamba shule 24 za sekondari zilizopo wilayani humo, uongozi wa wilaya hiyo
umejiwekea mkakati wa kujenga mabweni manne katika kila shule ili watoto wa
kike pia waweze kuishi huko na kuepukana na tabia ya kuzurula hovyo mitaani
jambo ambalo nalo huchangia waweze kupata ujauzito.
“Kila bweni moja litakalojengwa litakuwa na uwezo wa kubeba
watoto wa kike 150 kila kata husika tunahamasisha wananchi wafyatue tofari kwa
wingi ili kuweza kufanikisha ujenzi wa mabweni haya”, alisisitiza.
Amlima alifafanua kuwa katika kufanikisha ujenzi huo,
serikali nayo inao mchango wake katika ujenzi wa mabweni hayo ikiwemo kuchangia
vifaa vya kiwandani kama vile bati, nondo, misumari na saruji ili ujenzi
unaofanyika uweze kwenda kwa ufasaha na kuleta manufaa makubwa katika jamii.
Alibainisha kuwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi
Februari mwaka huu kwa wale waliofaulu kwenda sekondari 12 ambao ni watoto wa
kike wameshindwa kuendelea na masomo yao darasani kutokana na tatizo hilo, huku
28 ambao nao waliliripoti shuleni wamekatisha masomo yao kutokana na kuwa
wajawazito.
Kadhalika aliongeza kuwa serikali inao mpango wa kutoa elimu
kwa kila kata kwa wananchi katika kupambana na tatizo la kuwapa mimba watoto wa
kike wilayani Namtumbo hivyo wazazi wanapaswa kuona umuhimu wa kujenga
ushirikiano na serikali katika kupambana na tatizo hilo.
Pia Mkuu huyo wa wilaya, Amlima amezitaka taasisi za Polisi
na Mahakama wilayani humo waone kwamba kuna umuhimu wa kufuatilia suala hilo
kwa karibu, kwani taasisi hizo za umma alizinyoshea kidole akidai kuwa viongozi
wake wilayani humo wamekuwa ndio chanzo cha kukumbatia maovu katika kupambana
na tatizo hilo la mimba kwa watoto hao.
No comments:
Post a Comment