Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MWENYEKITI wa Mfuko wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Hyasint
Ndunguru amesema kuwa bodi hiyo hapa nchini, imetoa shilingi milioni 40 kwa ajili
ya kugharimia nusu ya bei ya miche bora ya kahawa kwa wakulima.
Ndunguru alisema kuwa gharama hiyo imelipwa kwa Taasisi ya Utafiti
wa zao la Kahawa Tanzania (TaCRI) ambao ndiyo wanaozalisha miche hiyo kwa gharama
ya shilingi 300 kwa kila mche mmoja wa kahawa.
Hayo yalisemwa na Mwenyekiti huyo katika kikao cha Wadau wa
kahawa Kanda ya Ruvuma kilichofanyika mjini Songea kwenye ukumbi wa Hanga,
ambapo wadau hao walikutana kwa lengo la kuhamasishana namna ya kudumisha ubora
wa zao la kahawa mkoani hapa.
“TaCRI tumekwisha walipa nusu ya bei ya kila mche wa kahawa
shilingi 150 hivyo mkulima atakapokwenda kununua mche wa kahawa kwenye kituo
cha taasisi hii popote pale kilipo anapaswa kulipia nusu nyingine ya bei ambayo
ni shilingi 150 tu kwa mche mmoja na sio vinginevyo”, alisema Ndunguru.
Alisema kuwa hayo yote yanafanyika kufuatia maazimio
yaliyowekwa na wadau wa kahawa ambayo yalipitishwa kitaifa katika vikao husika
kwamba asilimia 0.75 ya ushuru wa fedha yote inayopatikana kwenye minada ya
kahawa itumike kuisaidia serikali kwa shughuli za utafiti.
Vilevile aliongeza kuwa asilimia 0.2 imekuwa ikisaidia
gharama za uendeshaji katika shughuli za minada hiyo na kwamba kufuatia maazimio
hayo mfuko umeweza kupata hati safi kutokana na utendaji mzuri wa maazimio ya
wadau hao.
Kwa upande wao wadau wa zao hilo walipokuwa wakichangia hoja
kwa nyakati tofauti katika kikao hicho waliweka maazimio kwamba Bodi ya kahawa
Tanzania vilevile ikae na halmashauri za wilaya na kukubaliana kutumia takwimu
za uzalishaji wa kahawa za halmashauri husika katika ukokotoaji wa hesabu za
ushuru wa makato ya kahawa mnadani Moshi.
Pia walieleza kuwa bodi hiyo inapaswa itoe hati ya makato
hayo na kurejesha ushuru uliokatwa kwenye halmashauri hizo kwa wakati kwa
kuzingatia taratibu za mikataba husika.
Kadhalika naye Meneja wa TCB Kanda ya Ruvuma, Peter Bubelwa
aliwaeleza wadau hao kuwa ili kuongeza thamani ya ubora wa kahawa kuna kila
sababu sasa kwa wakulima kuendelea kuwahamasisha pia watumie mashine za CPU
ambazo huongeza ubora wakati wa ukoboaji wa kahawa mbivu kipindi cha msimu wa
mavuno ya zao hilo.
No comments:
Post a Comment