RAIS Dkt. John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika
sherehe za siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kitaifa, huku kilio kikubwa
cha vyama vya wafanyakazi kikiwa kukosekana kwa mikataba ya hali bora kazini.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Vyama Huru vya
Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Taifa lilipaswa kuwa na waajiriwa milioni 3.7
katika sekta iliyo rasmi, lakini waliopo ni 650,000 pekee, hali inayoashiria
kutokuwa na mikataba.
Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Yahaya Msigwa alisema hayo juzi
mjini Moshi ikiwa ni maandalizi ya Mei Mosi itakayofanyika Uwanja wa Chuo Kikuu
cha Ushirika Moshi (MoCU).
“Tayari tumemwandikia Rais Dkt. Magufuli kumuomba awe mgeni
rasmi, kimsingi sherehe zote kitaifa mgeni rasmi ni yeye............tunazo
ajenda za kumpa Rais, lakini moja ya mambo ambayo ni kero ni hili la mikataba
ya hali bora kazini, wafanyakazi wengi wanafanya kazi kama vibarua na hawajui
haki zao,” alieleza Msigwa.
Alitolea mfano wa watumishi wa mashambani pekee nchini Kenya
ni zaidi ya 700,000 na Afrika Kusini ni zaidi ya milioni moja na kwamba ipo
haja kwa waajiri Tanzania kutafakari upya suala la maslahi ya wafanyakazi wao
na Rais anapaswa kulisemea hilo.
Aidha, Katibu Mkuu huyo wa Tucta alitaka waajiri kuruhusu
kuundwa kwa mabaraza ya wafanyakazi sehemu za kazi ili kutoa fursa kwa
wafanyakazi kukutana na kujadili maslahi yao lakini pia kufanya kazi kwa tija
zaidi.
Katika hatua nyingine, Msigwa alisema Tucta inaunga mkono
kampeni ya serikali ya awamu ya tano ya kupambana na wafanyakazi hewa sanjari
na mpango wa kupunguza matumizi ya serikali.
“Pamoja na nia njema ya serikali katika kupambana na
wafanyakazi hewa, lakini tunaomba haki itendeke na isitokee mfanyakazi ameonewa
kwa namna yoyote ile kwani huko ni kuwakatisha tamaa wafanyakazi waadilifu na
waaminifu,” alisema.
Maadhimisho ya Mei Mosi yatahusisha pia kujengwa kwa mabanda
ya kuoneshwa kwa shughuli mbalimbali za kisekta hapa nchini.
No comments:
Post a Comment