Waziri Mhagama akikagua maandalizi ya kuadhimisha sherehe za miaka 53 ya Muungano katika viwanja vya Jamhuri leo mjini Dodoma. |
Na Immaculate Makilika,
Maelezo Dodoma.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu,
Ajira na Wenye ulemavu, Jenista Mhagama amewaasa Watanzania kuwa wazalendo
pamoja na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
Alisema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza mjini Dodoma
wakati akifuatatilia maandalizi ya maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano
yatakayofanyika Aprili 26 mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri uliopo mjini hapa.
“Tunapoadhimisha miaka 53 ya Muungano ninawaomba watanzania
kuwa wazalendo pamoja na kulinda amani ya nchi”, alisema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama aliwaomba watanzania hasa wakazi wa Dodoma,
kuhudhuria pia kwa wingi katika maadhimisho hayo yatakayofanyika Aprili 26
mwaka huu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana
alisema kuwa mkoa wake umejipanga vizuri katika kufanikisha maadhimisho hayo
ambapo pia alivishukuru vyombo vya habari kwa kuhamasisha wananchi juu ya sherehe
hizo.
“Wananchi wamehamasika kushiriki katika maadhimisho haya ya
miaka 53 ya Muungano, ninawashukuru kwa kazi kubwa mliyoifanya na tunaamini
mtaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika maadhimisho haya”, alisema.
Maandalizi ya maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano
yamehudhuriwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Christina Mndeme pamoja na
viongozi mbalimbali wa Serikali.
Aidha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, ambapo pia
yatahudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali
Mohamed Shein na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.
Maadhimisho hayo ya miaka 53 ya Muungano yanatarajiwa
kupambwa na maonesho kutoka kutoka vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama,
burudani za vikundi vya ngoma pamoja na maonesho ya halaiki.

No comments:
Post a Comment