Na Julius Konala,
Songea.
MBUNGE wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas Gama
ametoa mkopo wa shilingi milioni 13 kwa ajili ya vikundi mbalimbali 26 vya
ujasiriamali jimboni humo, kwa lengo la kuvisaidia kukua kiuchumi ili waweze
kuondokana na umaskini.
Akikabidhi hundi hizo mwishoni mwa wiki kwa viongozi wa vikundi vya
ujasiriamali kwa niaba ya Mbunge huyo katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya
Songea, Mkuu wa wilaya ya Songea Palolet Mgema amewataka wajasiriamali hao
kutumia mikopo hiyo kwa kazi iliyokusudiwa.
Mgema aliwaonya wajasiriamali hao kuacha tabia ya kutumia
fedha hizo kwa mambo ya anasa ikwemo kwenye mambo ya ulevi, mashindano ya kuvaa
nguo pamoja na kucheza mchezo wa kupeana jambo ambalo alidai kuwa kufanya hivyo
kunaweza kusababisha wakashindwa kurejesha mkopo huo kwa wakati.
Aidha alimpongeza Mbunge wa jimbo hilo, Gama kwa kutoa mkopo
huo kwa vikundi hivyo vya ujasiriamali kwani kufanya hivyo ni sawa na
kuwaongezea safari ya kukuza mitaji yao na kuwainua kiuchumi katika shughuli
zao za kimaendeleo.
Naye Katibu wa Mbunge huyo, Kassian Mbawala alisema kuwa
lengo la Mbunge huyo ni kutoa mikopo hiyo kwa vikundi vya ujasiriamali na
kutaka kuviwezesha ili viweze kujiinua kiuchumi ikizingatiwa kwamba mkoa wa
Ruvuma, upo nyuma kimaendeleo kwa kuwa na viwanda ambapo amedai kuwa kila kikundi kitanufaika na
mkopo huo kwa kupewa shilingi 500,000.
Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano ya hundi hizo Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Songea mjini, Gerlod Mhenga alidai kuwa
kitendo kilichofanywa na Gama ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho
na ahadi aliyoitoa katika kampeni zake wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Songea, Abdul Mshaweji
akizungumza katika hafla hiyo ameishukuru ofisi ya Mbunge kwa kutoa mkopo huo kupitia
mfuko wa jimbo na kwamba amewataka wajasiriamali hao kuutumia vizuri ili waweze
kupiga hatua mbele na kuelekea katika malengo yao ya kuunda SACCOS yao.
Kwa upande wao baadhi ya wajasiriamali walionufaika na mkopo
huo Anna Mlimila na Mohamed Gayo wamemshukuru Mbunge huyo kwa mkopo alioutoa
huku wakiahidi kuutumia vizuri kwa kazi na malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kwa
ajili ya kukuza mitaji yao.
No comments:
Post a Comment