Ofisa unasihi na upimaji wa shirika la Health Promotion Tanzania (HDT) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, Zawadi Mtambo. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Health Promotion Tanzania
(HDT) lililopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, ambalo linajishughulisha na udhibiti
wa maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) limefanikiwa kuwarudisha watu 1,229
ambao walipotea kumeza dawa za kufubaza virusi vya ugonjwa huo na kuwarudisha
katika Vituo vya tiba (CTC) kwa ajili ya kupata huduma endelevu.
Aidha kati ya hao taarifa za awali zinaonesha kuwa katika
kipindi cha mwaka jana kulikuwa na wagonjwa 717 waliopotea ambapo HDT
walifanikiwa kuwarudisha wagonjwa 507 ambao sasa wanaendelea kumeza dawa hizo.
Kadhalika katika kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi
mwaka huu kulikuwa na wagonjwa 1,684 waliopotea na sasa wamerudishwa wagonjwa
722 hivyo zoezi hilo utekelezaji wake umefikia asilimia 42.9 ambapo malengo ya
shirika katika utekelezaji huo ni kufikia asilimia 80 na kwamba kazi hiyo bado
inaendelea.
Dkt. Joachim Henjewele ambaye ni Meneja Mkuu wa shirika
lisilokuwa la kiserikali la Health Promotion Tanzania (HDT) lililopo Mbinga
mjini, ambalo linajishughulisha na udhibiti wa maambukizi mapya ya VVU alisema
hayo juzi wakati alipokuwa akihojiwa na waandishi wa habari ofisini kwake.
Dkt. Henjewele alisema kuwa shirika hilo lilikuja Mbinga kwa
sababu ya kuwa na taarifa za awali kwamba kuna maambukizi makubwa ya virusi vya
ugonjwa huo ambapo hivi sasa wamekuwa wakiendelea na zoezi la upimaji wa hiari.
Pamoja na mambo mengine Ofisa huyo alieleza pia HDT wamekuwa
wakipinga masuala ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, elimu ya lishe imekuwa
ikitolewa kwa watu wanaoishi na Virusi vya ukimwi pamoja na elimu ya kujikwamua
kiuchumi kwa makundi ya watu wanaoishi na ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment