Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
UMETOKEA ugonjwa wa nguruwe aina ya African Swain Fever,
katika kijiji cha Kitura kata ya Kitura wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma na
kusababisha nguruwe 18 kufa katika kijiji hicho, baada ya kuripotiwa wakiwa na
ugonjwa huo.
Aidha imeelezwa kuwa chanzo cha ugonjwa huo kutokea
kijijini hapo umesababishwa na mama mmoja ambaye hakutajwa jina lake akitokea
mkoa wa Njombe, baada ya kusafirisha nyama ya nguruwe na kupeleka katika kata
hiyo kwa lengo la kubadilishana na zao la kahawa kwa wananchi wanaoishi huko.
Hayo yalisemwa jana na Daktari Mkuu wa mifugo
halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Patrick Banzi wakati alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake huku akieleza kuwa hauna madhara kwa binadamu
lakini endapo ukiingia sehemu yoyote ile yenye wanyama hao umekuwa ukiua
nguruwe wengi kwa muda mfupi.
“Ugonjwa huu ukiingia kwenye zizi kama kulikuwa na hata
nguruwe 100 wote wanakufa mara moja, hivyo tumezuia uchinjaji kuendelea katika
maeneo yote yaliyoathirika katika kijiji kile”, alisema Dkt. Banzi.
Pia aliongeza kuwa katika kupambana na ugonjwa huo wa
African Swain Fever kwenye maeneo ya kata hiyo ya Kitura, tayari dawa
zimepulizwa na wanyama wote waliokufa wamefukiwa.
Dkt. Banzi alifafanua kuwa vilevile wamezuia kwa kutoruhusu
kuingiza mifugo au kutoa ndani ya wilaya ya Mbinga, ikiwemo nyama na mbolea za
samadi zitokanazo na mnyama huyo.
Alisisitiza kuwa kwa wale wote wanaojishughulisha na
uchinjaji wanapaswa pia kuwa na vibali maalumu vya uchinjaji, ambavyo vinawatambulisha
wapi wanatoka na mifugo na mifugo yao kuchunguzwa kitaalamu ili isiweze kuleta
madhara kwa wengine.
Pamoja na mambo mengine nazo serikali za vijiji wilayani
humo zimesisitizwa kutenga maeneo maalumu ya uchinjaji na kwamba kwa wale wote
watakaokiuka utaratibu huo watatozwa faini ya shilingi 300,000 na isiyozidi
500,000 au kushtakiwa mahakamani na kwenda jela kifungo cha miezi sita au vyote
kwa pamoja.
No comments:
Post a Comment