Na Muhidin Amri,
Nyasa.
BAADHI ya wananchi wanaoishi
katika vijiji vya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma,
wameiomba serikali kupitia Jeshi la Polisi wilayani humo kufanya doria ya mara
kwa mara kando kando mwa ziwa Nyasa, ili kuweza kuwachukulia hatua watu wenye mazoea ya kuoga ziwani
wakiwa uchi wa mnyama.
Walisema kuwa tabia hiyo imekuwa ikichochea na kuchangia kwa
kiasi kikubwa ongezeko la vitendo vya ngono zembe, miongoni mwa baadhi ya wananchi
wanaoishi wilayani humo na kusababisha maambukizi mapya ya Virusi Vya
Ukimwi (VVU).
Kelvin Komba (42) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nkiri
wilayani hapa alisema kwamba katika wilaya hiyo hususani vijijini kwenye
makambi ya wavuvi, wanaume na wanawake wamekuwa na tabia hiyo tena huoga bila
nguo huku wakiwa jinsia tofauti.
Komba alieleza kuwa vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha watu
hao hasa wanaume ambao hukaa kwenye makambi hayo kwa muda mrefu bila kukutana
na wenzi wao, hushikwa na tamaa ya ngono na kujikuta wakifanya tendo hilo bila
kuchukua tahadhari ya kutumia kinga.
Naye Rehema Nchimbi kutoka katika mji wa Mbamba bay wilayani
Nyasa alisema hata katika maeneo yenye mkusanyiko wa watu wengi yaani wanawake
na wanaume kumekuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU, licha ya juhudi kubwa
zinazofanywa na serikai katika kukabiliana na maambuzi hayo yakiwemo magonjwa
mengine ya zinaa.
Alisema kuwa katika maeneo hayo ya wavuvi hata baadhi ya vijiji
vingine watu hupendelea kuchanganyika na watoto wadogo bila kujali umri, hivyo
umefika wakati sasa hata kwa viongozi wa serikali za vijiji kuchukua hatua kwa
kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo isiweze kuendelea kwani inakiuka maadili ya
kitanzania.
Pamoja na mambo mengine wameiomba serikali kuchukua hatua
madhubuti ya kukomesha tabia hiyo na kupeleka elimu juu ya madhara ya kufanya
hivyo ikiwemo gonjwa la ukimwi, hasa katika kambi za wavuvi hao ambako ndiko kumeshamiri
vitendo hivyo ili kuweza kunusuru maisha ya watu wengi hasa vijana ambao ni
nguvu kazi ya taifa hili.
No comments:
Post a Comment