Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya mji wa Mbinga, wakijadiliana jambo mara baada ya kuhitimisha kikao chao cha baraza la Madiwani kilichoketi juzi mjini hapa. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
WANANCHI wanaoishi katika
halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wamesisitizwa kuwa na mazoea ya
kutumia Kondomu wakati wa kufanya tendo la ndoa ili kuweza kupunguza kasi ya maambukizi
ya Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Vilevile kutokana na
maambukizi hayo kuendelea kushika kasi katika mji huo, halmashauri hiyo imejiwekea
utaratibu wa kusambaza Kondomu hizo katika maeneo ya starehe na kutoa elimu kwa
wananchi kupitia mikutano mbalimbali namna ya kuepukana na maambukizi hayo.
Hayo yalisemwa juzi na Kaimu
Afisa maendeleo ya jamii wa mji huo, Alphonce Njawa wakati alipokuwa akitoa
taarifa ya maendeleo ya Kamati ya kudhibiti ugonjwa wa ukimwi katika
halmashauri hiyo.
Njawa alisema kuwa utekelezaji
wa kazi za kitengo cha ukimwi, kinga na tiba kwa kipindi cha Januari hadi Machi
mwaka huu wameweza kufanya mikutano ya tahadhari juu ya mila na desturi potofu
zinazochochea kuenea kwa maambukizi mapya ya ugonjwa huo hasa kwa watu
waliokuwa kwenye ndoa.
Pia kwa ushirikiano na kitengo
cha ustawi wa jamii elimu imetolewa kwa watu walio kwenye mahusiano ya ndoa ambao
wanapeleka malalamiko yao mbalimbali juu ya unyanyasaji wa kijinsia
wanaofanyiwa na waume zao ikiwemo utelekezwaji wa familia na wale wanaotaka
kuachana wapatao 353 katika kipindi hicho wamepewa huduma hiyo.
“Kondomu pisi 864 zimetolewa
kwa wanaume na wanawake katika kipindi hiki hasa kwa wale wanaokuja kuleta
malalamiko ofisini, watu waliokuwa maofisini na madereva wa pikipiki maarufu
kwa jina la boda boda sambamba na elimu juu ya matumizi sahihi ya kondomu hizo”,
alisema Njawa.
Kadhalika kwa upande wao
Madiwani wa halmashauri ya mji wa Mbinga walipongeza jitihada hizo zinazofanywa
na kamati hiyo huku wakisisitiza kuwa ziendelezwe kwani ugonjwa huo umekuwa
ukienea kwa kasi na kuendelea kutesa watu.
No comments:
Post a Comment