Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, limewafukuza kazi watumishi wake wa nne kutoka idara
mbalimbali wilayani humo na wengine kupewa onyo kali baada ya kubainika kuwa na
makosa ya uzembe na ubadhirifu wa mali za umma.
Akitoa taarifa hiyo ya
kufukuzwa kazi watumishi hao katika kikao cha baraza hilo kilichoketi juzi
kwenye ukumbi wa Umati mjini hapa, Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo
Benward Komba alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kubainika kuwa wamekuwa
na mazoea ya kufanya makosa hayo mara kwa mara.
Komba aliwataja watumishi hao
kuwa ni aliyekuwa afisa mtendaji wa kata ya Kitura, Daniel Komba ambaye
amefukuzwa kazi kutokana na kufanya matendo kinyume na dhamira njema ambapo alifoji
risiti za marejesho ya fedha shilingi 350,000 ambazo ni michango ya wananchi wa
kata hiyo.
Alibainisha kuwa fedha hizo
walikuwa wamechanga wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo yao ambapo
alizitafuna kwa manufaa yake binafsi na halmashauri ilipofanya ufuatiliaji wa
kina ilibaini kwamba risiti aliyoitumia kukusanyia fedha hizo haikuwa risiti
halali ya serikali.
Vilevile aliwataja wengine
kuwa ni Ramadhan Mang’una ambaye ni afisa kilimo msaidizi, Allan Ndunguru afisa
mtendaji wa kijiji cha Ulima na Michael Nakitundu naye ni afisa mtendaji wa
kijiji cha Ulolela ambao nao walishiriki kufanya ubadhirifu wa mali za umma
katika vijiji hivyo.
Pia katika hatua nyingine
baraza hilo la Madiwani lilitoa onyo kali kwa watumishi wengine wanne ambao nao
walisimamishwa kazi na kufanyiwa uchunguzi wakituhumiwa kushiriki kufanya
ubadhirifu wa mali za halmashauri hiyo na kubainika kwamba baada ya uchunguzi
huo kukamilika hawakuwa na hatia hivyo wamerejeshwa kazini.
Watumishi hao walitajwa kuwa
ni Sidney Mpangala ambaye ni mchumi kutoka idara ya mipango, David Davis afisa
manunuzi, Onesmo Mapunda afisa mipango wa wilaya na Edward Kadege fundi sanifu
idara ya ujenzi.
Hata hivyo awali
waliposimamishwa kazi walikuwa wakituhumiwa kufanya ubadhirifu na wizi wa mali
za umma katika kazi ya ujenzi wa kibanda cha mlinzi chenye thamani ya shilingi
milioni 19,000,000 kwenye nyumba ya kuishi Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo
ambayo imejengwa mtaa wa Kipika mjini hapa.
No comments:
Post a Comment